1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaBrazil

Lula ahimiza upatanishi wa pamoja wa vita vya Ukraine

16 Aprili 2023

Rais wa Brazil Luis Inacio Lula da Silva amesema hii leo kwamba amejadiliana na China na Umoja wa Falme za Kiarabu juu ya kuwepo kwa upatanishi wa pamoja katika vita vya Urusi nchini Ukraine.

https://p.dw.com/p/4Q9KO
Rais wa Brazil Luis Inacio Lula da Silva akiwa na rais wa UAE Sheikh Mohamed bin Zayed al-Nahyan(Kulia) wakati Lula alipozuru taifa hilo.
Suala la ushirikiano katika kuvimaliza vita vya Ukraine linahimizwa sasa miongoni mwa mataifa yanayotaka amani nchini humo.Picha: UAE'S MINISTRY OF PRESIDENTIAL AFFAIRS/AFP

Rais wa Brazil Luis Inacio Lula da Silva ametoa wito huo, wakati kwa upande mwingine akiishutumu Marekani na Ulaya kwa kuurefusha mzozo huo kutokana na kuendelea kupatia Ukraine silaha.

Lula aliyekuwa kihitimisha ziara yake rasmi nchini China na Umoja wa Falme za Kiarabu amewaambia waandishi wa habari akiwa Abu Dhabi kwamba, mataifa hayo mawili na mengine yanapaswa kuungana na kundi la kisiasa la G20 katika kujaribu kuvimaliza vita hivyo.

Lula amesema amezungumza na Mtawala wa Umoja wa Falme za Kiarabu, Sheikh Mohammed bin Zayed Al Nahyan na rais wa China Xi Jinping juu ya kuunda kundi la mataifa ya mazungumzo ya upatanishi, kutoka katika kundi la mataifa yaliyoendelea ya G20 na kuongeza kuwa hiyo ndio nia yake na anaamini watapata mafanikio makubwa.

Lula aidha amesema tayari amejadiliana suala hilo na rais wa Marekani Joe Biden, kansela wa Ujerumani Olaf Sholz, rais wa Ufaransa Emmanuel Macron pamoja na wakuu wa baadhi ya mataifa ya Marekani Kusini.