1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Lubanga arejea nyumbani DRC, apokewa kishujaa

11 Septemba 2020

Baada ya kukaa jela kwa kipindi cha zaidi ya miaka 16 kutumikia adhabu ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, kiongozi wa zamani wa waasi wa UPC, Thomas Lubanga, amerejea nyumbani aliopokelewa na maelfu ya raia.

https://p.dw.com/p/3iKsO
Den Haag Internationaler Strafgerichtshof Thomas Lubanga 19.05.2014
Picha: Reuters

Maelfu ya watu walijokeza mjini Bunia kumpokea Thomas Lubanga, ambae baadhi ya watu wa kabila lake la Bahema wamembatiza jina la Nelson Mandela wa Ituri.

Édouard Unwanga Balladur, mmoja wa wazee wa busara wa kabila la Alur, aliiambia DW kwamba Lubanga "alipatishwa tabu ya bure na ilhali alikuwa akifanya jambo kwa manufaa ya wakaazi wa Ituri", alipokuwa kiongozi wa kundi la waasi wa Muungano wa Wazalendo wa Congo, UPC.

Lubanga, aliyewasili Bunia baada ya kuwa gerezani nchini Uholanzi kwa muda wa miaka 14, sasa anakabiliwa na kibarua kigumu cha kuyapatanisha makabila ya Bahema na Lendu, kufuatia mauwaji yanayoendelea katika wilaya ya Djugu.

Kongo 2003 Rebellen UPC
Sehemu ya kundi la waasi wa UPC ambao wakiongozwa na Thomas Lubanga.Picha: AP

Mauwaji hayo yanayofanywa na waasi wa CODECO wanaotokea kabila la Walendu na yanayowalenga watu wa kabila la Bahema hayajatajwa hadi sasa kuwa ni mauwaji ya kikabila. 

Kuwasili kwa Lubanga kumesadifiana pia na kipindi cha maombolezo kwa watu wa Ituri kufuatia mauaji ya wenzao wapatao 50 yaliyofanywa na waasi wa kundi la ADF katika vijiji vya Belu, Payipayi na Katanga, katika wilaya ya Irumu, kusini mashariki ya Bunia, wilaya inayopakana na wilaya ya Beni katika mkoa jirani wa Kivu ya Kaskazini. 

Waasi wa ADF, ambao wanafanya mauwaji kila uchao katika wilaya ya Beni, kwa sasa wanafanya mauwaji hayo hayo katika vijiji mbalimbali vya mkoa wa Ituri.

Serikali kuu mjini Kinshasa imetuma ujumbe wake mjini Bunia unaoongozwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Ndani, Gilbert Kankonde, kutathmini yanayojiri huko.

Imetayarishwa na John Kanyunyu/DW Beni