1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

London . AI yataka Burma kuwekewa vikwazo vya silaha.

2 Oktoba 2007
https://p.dw.com/p/CBL0

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limetoa wito kwa baraza la usalama la umoja wa mataifa kuiweka vikwazo vya silaha dhidi ya Burma.

Shirika hilo pia limeyataka mataifa makuu yanayoiuzia Burma silaha China na India , kusitisha mauzo yote, na kusema vikwazo hivyo viendelee hadi pale utawala wa kijeshi wa Burma utakapoboresha haki za binadamu. Utawala huo wa kijeshi ulizima vuguvugu la kudai demokrasia wiki iliyopita wakati majeshi ya serikali yalipotumia risasi , mabomu yenye gesi ya kutoa machozi, na virungu kuwaondoa waandamanaji kutoka mitaani. Mamia ya watu , ikiwa ni pamoja na watawa wa dini ya Kibudha , walikamatwa kutokana na kushiriki kwao katika maandamano. Serikali inasema kuwa watu 10 wameuwawa katika mapambano hayo, lakini duru huria zinasema kuwa idadi inaweza kuwa ya juu zaidi.

Wakati huo huo , shirika la habari la Associated Press limeripoti kuwa mjumbe wa umoja wa mataifa Ibrahim Gambari anatarajiwa kukutana na jenerali mkuu wa jeshi la Burma , Than Shwe leo. Siku ya Jumapili , Gambari alikutana na kiongozi wa upinzani Aung San Suu Kyi, katika juhudi za kutafuta suluhisho la amani katika ghasia za nchi hiyo.