1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Licha ya kufutiwa mashitaka,Trump bado aendelea kuandamwa

16 Februari 2021

Kiongozi mwandamizi wa Democratic Nancy Pelosi ametangaza uchunguzi huru kuhusiana na uvamizi wa jengo la bunge uliofanywa na wafuasi wa Trump mwezi Januari. Baadhi ya Warepublican wameunga mkono wazo hilo.

https://p.dw.com/p/3pQ6g
USA Ohio US-Präsident Donald Trump
Picha: Reuters/J. Ernst

Warepuplican wengi katika baraza la Senate nchini Marekani walipiga kura ya kumfutia mashitaka Donald Trump katika kesi ya kumshtaki wiki iliyopita, lakini matatizo ya rais huyo wa zamani bado hayajaisha. 

Spika wa baraza la wawakilishi Nancy Pelosi ametoa wito wa kuundwa tume kama ile ya baada ya mashambulizi ya kigaidi ya Septemba 11, ili kuchunguza shambulizi la Januari 6 katika jengo la bunge la Marekani la Capitol lililofanywa na wafuasi wa Trump.

Pelosi amesema tume hiyo italenga kutathmini ukweli na sababu za uvamizi huo wa bunge, akisisitiza kuwa lazima ukweli upatikane kuhusu kilichotokea.

Matamshi ya Pelosi yanakuja baada ya Baraza la Seneti Jumamosi iliyopita kupiga kura kumuondolea mashitaka Trump kuhusiana na jukumu lake katika tukio hilo.

Baadhi ya Warepublican pia wametoa wito wa kuundwa tume hiyo mfamo wa ile ya Septemba 11. Lindsey Graham, seneta Mrepublican kutoka jimbo la South California na mfuasi sugu wa Trump, amesema uchunguzi huo utahitajika ili kulilinda vyema zaidi jengo la Bunge dhidi ya uvamizi wa aina hiyo katika siku za usoni.

USA Trump Impeachment Nancy Pelosi
Kiongozi mwandamizi Nancy Pelosi ambaye ameitisha uchunguzi juu ya uvamizi wa majengo ya bungePicha: Manuel Balce Ceneta/AP Photo/picture alliance

Ijapokuwa Trump alifutiwa mashitaka ya kuchochea uvamizi wa bunge katika kesi iliyofanywa na Seneti, baadhi ya Warepublican wamedai kuwa rais huyo wa zamani anaweza bado kushitakiwa mahakamani. Kiongozi wa Warepublican katika Seneti Mitch McConnell, Mrepublican kutoka Kentucky, alisema hakuna swali kuwa Trump anahusika kivitendo na kimaadili na vurugu zilizotokea bungeni Januari 6.

Mwanasheria mkuu aliyependekezwa na Biden Merrick Garland, amehimizwa na shirika moja maarufu la siasa za mrengo wa kushoto kumfungulia mashitaka Trump na washirika wake kutokana na kuhusika kwao katika uvamizi wa jengo la bunge na uhalifu mwingine. Baada ya Trump kuondolewa mashitaka Jumamosi, shirika hilo la Progressive Change Campaign Committee - PCC ilisambaza ombi la kumshinikiza Garland kumchunguza Trump.

Taarifa ya kundi hilo ilisema, kama tunataka Trump awajibishwe na mtandao wake wa uhalifu, hatuwezi tu kuwategemea viongozi wa Democratic.

Mwanasheria mkuu wa New York Letitia James, pamoja na Mwanasheria wa wilaya ya Manhattan Cyrus Vance Jr. tayari wameanzisha uchunguzi tofauti wa uhalifu kuhusiana na biashara za Trump. Kwa sasa haifahamiki kama James au Vance atafungua mashitaka ya uhalifu dhidi ya Trump sasa baada ya kuondoka madarakani.