1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Utawala wa sheriaAfrika

Liberia yamfuta kazi Gavana wa Benki Kuu

31 Julai 2024

Gavana wa benki kuu ya Liberia amekufuzwa kazi baada ya ukaguzi uliofanywa kuonesha hitilafu za mahesabu katika utoaji mikopo kwa serikali na matumizi ambayo hayakuidhinishwa.

https://p.dw.com/p/4ivrv
Liberia | Rais Joseph Boakai
Rais Joseph Boakai wa Liberia.Picha: Olamikan Gbemiga/AP Photo/picture alliance

Waziri wa mawasiliano wa Liberia na msemaji wa benki kuu ya nchi hiyo wamesema Gavana Jolue Aloysius Tarlue anaondolewa kazini mara moja baada ya kutolewa ripoti ya ukaguzi iliyochunguza hesabu kati ya mwaka 2018 hadi 2023.

Ukaguzi huo ulianzishwa kwa amri ya Rais Joseph Boakai aliyeingia madarakani mnamo mwezi Januari.

Umebaini dosari kwenye chombo hicho kinachosimamia sera za uchumi wa taifa ikiwemo mkopo wa dola milioni 80 uliotolewa kwa serikali kinyume cha utaratibu. Kasoro nyingine ni utoaji wa kandarasi pamoja na matumizi ya fedha ambazo hazikuidhinishwa kisheria.

Liberia ni mojawapo ya nchi zenye viwango vya chini vya uwazi katika matumizi ya fedha umma na mapambano dhidi ya ufisadi, hayo ikiwa ni kulingana na faharasa inayotathmini viwango hivyo duniani.