1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Leverkusen waangazia macho fainali mbili zilizobaki

20 Mei 2024

Mabingwa wa kihistoria wa Bundesliga Bayer Leverkusen wameanza leo mazoezi ya mechi zao mbili za kuukamilisha msimu. Fainali ya Ligi ya Ulaya dhidi ya Atalanta na fainali ya DFB Pokal dhidi ya Kaiserslauten.

https://p.dw.com/p/4g4Up
Mabingwa wa Bundesliga Leverkusen
Leverkusen wameshinda ubingwa wa Bundesliga kwa mara ya kwanza katika historia yaoPicha: Wolfgang Rattay/REUTERS

Leverkusen ndio timu ya kwanza kuumaliza msimu wa ligi kuu ya kandanda Ujerumani – Bundesliga bila kupoteza mechi, na wamefanya hivyo katika ubingwa wao wa kwanza wa ligi. Ikumbukwe kuwa hajawapoteza mchuano wowote katika mashindano ya Ligi ya Ulaya – Europa League na Kombe la Shirikisho la Ujerumani – DFB Pokal ambapo watacheza fainali na Atalanta Jumatano wiki hii, na kushuka dimbani Jumamosi ijayo dhidi ya Kaiserslauten.  

Kocha Xabi Alonso alishangilia mbele ya mashabiki walioimba jina lake uwanjani baada ya kipenga cha mwisho. "Ninajivunia sana sana. Unajua....kuwa bingwa wa Bundesliga ni ngumu sana lakini kufanikisha hilo bila kupoteza mechi ni mara ya kwanza, kwa hivyo inanifanya nijivunie sana. Nawashukuru sana wachezaji kwa juhudi zao zote, kwa maandalizi yao yote, kwa uthabiti wote ambao tumeonyesha. Na hiyo ina maana kubwa na kwa hakika, hatutasahau hilo na mashabiki wengi wa soka hawatasahau.”

Kocha wa Leverkusen Xabi Alonso
Xabi Alonso alijiunga na Leverkusen akitokea Real Sociedad B ya Uhispania Picha: Michael Probst/AP Photo/picture alliance

Leverkusen wamefikisha mechi 51 katika mashindano yote bila kupoteza, ambayo tayari ni rekodi ya Ulaya, na hakuna timu yoyote iliyowahi kumaliza msimu bila kupoteza mechi katika mashindano yote

Reus awanunulia bia mashabiki

Katika dimba la Signal Iduna Park, mashabiki walimuaga shujaa wao Marco Reus ambaye alicheza mechi yake ya mwisho ya Bundesliga katika uzi wa Borussia Dortmund baada ya miaka 12 katika klabu hiyo. Na Reus mwenye umri wa miaka 34 aliwaaga kwa kuwanunulia bia.

Lakini kabla ya kuwapa kiburudisho cha bia, aliwaburudisha uwanjani kwa kufunga bao na kutoa asisti ya jingine katika ushindi wa 4 – 0 dhidi ya Darmstadt.

Marco Reus
Reus ameitumikia Borussia Dortmund kwa miaka 12 na anaondoka bila kubeba taji la BundesligaPicha: Moritz Müller/IMAGO

Dortmund walimaliza katika nafasi ya 5 lakini wanajiandaa kwa fainali ya LIGI ya Mabingwa dhidi ya Real Madrid Juni mosi dimbani Wembley mjini London. Nahodha Reus anasema watajiandaa kupambana "Huwezi kujua katika fainali. Unahitaji kuwa na siku nzuri. Sisi tunaisubiri sana siku hiyo. Tunahitaji kupambana vilivyo. Ni mchezo mmoja, na lolote linawezekana katika mchezo mmoja. Tutaona… Tunatumahi tunaweza kuwa na sherehe ya kweli mjini Dortmund siku inayofuata."

Soma pia: Bayer Leverkusen wametinga nusu fainali ya Ligi ya Ulaya

Stuttgart waliwapiku Bayern Munich katika nafasi ya pili matokeo ambayo yalionesha dhahiri matatizo yanayowakabili miamba hao wa Bavaria ambao wamemaliza msimu bila taji lolote kwa mra ya kwanza tangu mwaka wa 2012.

Katika vita vya kushuka daraja, Union Berlin walinusurika chupuchupu kupitia faida ya magoli na sasa watacheza katika Bundesliga msimu ujao, wakati Bochum watacheza mechi ya mchujo ya mikondo miwili dhidi ya Fortuna Düsseldorf iliyomalita katika nafasi ya tatu kwenye daraja la pili. St Pauli na Holstein Kiel zilipanda daraja wakati Koeln na Darmsdat zikishuka.

afp, ap, dpa, reuters