1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Lebanon yatangaza serikali mpya lakini maandamano yaendelea

22 Januari 2020

Lebanon imetangaza serikali mpya katika juhudi za kumaliza maandamano ambayo yamedumu kwa miezi kadhaa. Lakini maandamano na vurugu zimeendelea kushuhudiwa hata baada ya serikali mpya kutangazwa.

https://p.dw.com/p/3Wcnj
Libanon neuer Premierminister Hassan Diab
Picha: Reuters/M. Azakir

Waziri Mkuu Hassan Diab mwenye umri wa miaka 60 alitangaza baraza lake la mawaziri 20, wengi wakiwa wataalam wanaoungwa mkono na kundi la Hezbollah na vyama washirika kisiasa.

Hata hivyo, serikali hiyo ambayo imeundwa miezi mitatu baada ya aliyekuwa waziri mkuu Saad Hariri kujiuzulu, imepingwa na waandamanaji wanaotaka mageuzi kamili na serikali iundwe na wataalam huru wasioegemea upande wowote kisiasa wanaoweza kusuluhisha mgogoro mbaya zaidi wa kiuchumi na kifedha ambao umelikumba taifa hilo.

Diab amewapongeza Walebanon kwa juhudi zao kutaka mageuzi na kuboresha huduma nchini humo. Huku akisema kuwa sasa ni muda wa kufanya kazi, amewahakikishia wananchi kuwa serikali yake itashughulikia matakwa yao.

"Hii ndiyo mara ya kwanza, Lebanon imekuwa na serikali kama hii katika historia yake. Ni timu ya uokoaji, ambayo wajibu wake pekee ni kufanya kazi kwa bidii na kujitolea kikamilifu.” Amesema Diab.

Waandamanaji wakosoa vyama vya siasa

Lakini maelfu ya waandamanaji walijitokeza mitaani na kuziba barabara katika mji mkuu Beirut na maeneo mengine nchini humo wakilalamika kuwa makundi ya kisiasa bado yamehusika katika kuwatangaza mawaziri wapya, hata kama ni wataalamu na wasomi.

Waandamanaji nchini Lebanon wamekuwa wakitaka mageuzi kamili na mawaziri wasiegemee upande wowote wa kisiasa.
Waandamanaji nchini Lebanon wamekuwa wakitaka mageuzi kamili na mawaziri wasiegemee upande wowote wa kisiasa.Picha: picture-alliance/AP Photo/H. Ammar

Baadhi ya waandamanaji wamerusha mawe karibu na bunge hivyo kuwalazimisha polisi kuwatawanya kwa kuwafyatulia gesi ya kutoa machozi pamoja na maji ya kuwasha.

"Tunataka serikali ya wataalam, haikupaswa kuwajumuisha washauri wao. Wanamfanya nani mjinga? Tumekuwa tukiandamana kwa siku 90 na hatufurahi kufunga barabara.” Amesema Fadi Zakour ambaye ni miongoni mwa waandamanaji.

Guterres aukaribisha uundaji wa serikali mpya Lebanon

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephanie Dujarric amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameukaribisha uundaji wa serikali mpya na anatarajia kufanya kazi kwa ushirikiano na Diab pamoja na baraza lake la mawaziri.

Serikali iliyotangazwa ina wasomi na wataalamu akiwepo mwanamke Zeina Akar ambaye ni waziri wa ulinzi na pia ni naibu wa Waziri Mkuu miongoni mwa wanawake wengine sita. Hata hivyo  mawaziri hao walitangazwa na vyama vya kisiasa ambavyo waandamanaji wanasema havikutilia maanani matakwa yao.

Wachambuzi wanasema, serikali hiyo mpya inayoegemea kundi la Hezbollah linaloungwa mkono na Iran, huenda itapata ugumu kupata uungwaji mkono unaohitajika kitaifa, kikanda na hata kimataifa ili kuepusha uchumi kuporomoka.

Vyanzo: APE, AFPE