Lebanon: Wanawake katika siasa za kiukoo
28 Mei 2009Katika uchaguzi wa bunge la Lebanon hapo Juni 7, wanawake wanawakilisha mbili asilimia tu ya watetezi, wengi wao wakiwa na majina ya familia zilizokuwa zikionekana kwa vizazi na vizazi katika vikaratasi vya uchaguzi wa nchi hiyo. Majina kama ya Geagea, Hariri, Zwein na Tueni yanajulikana huko Lebanon kama yalivyo ya Gandhi huko India au Kennedy nchini Marekani. Katika siasa za Lebanon zilizojaa mitikisiko, kifo au kuuliwa mwanamume katika familia mara nyingi huwa ni sababu ya mwanamke katika familia hiyo kusukumwa aingie katika jukwaa la siasa, na yote ni kuhifadhi uridhi wa familia.
Kuna msemo ulio maarufu huko Lebanon kwamba njia pekee kwa mwanamke katika nchi hiyo kuingia bungeni ni kuvaa kanzu nyeusi ya maombolezi. Kwa wanawake kuweza kuwa watetezi katika uchaguzi wa Lebanon uliojengeka katika mfumo wa madhehebu ya kidini, ambako viti vya bunge vinagawiwa kwa mujibu wa madhehebu ya dini, wanawake wanahitaji waungwe mkono kisiasa, wasaidiwe kifedha, na zaidi, kuwa na maingiliano mazuri na koo zao.
Mtetezi wa kike anayetarajiwa kushinda kiti pekee kilichotengwa kwa ajili ya watu wa madhehebu ya Greek Orthodox katika eneo linalokaliwa na Wakristo wengi ni Nayla Tueni. Baba wa Nayla, Gebran, aliuliwa miezi sita baada ya kuchaguliwa mwaka 2005 kwa kiti ambacho bibi huyo anakiwania hivi sasa. Nayla ni makamo wa meneja wa gazeti la an-Nahar linaloongoza mjini Beirut na ambalo lilianzishwa na babu yake, na baadae kuhaririwa na kuchapishwa na marehemu baba yake. Gazeti hilo linaungwa mkono na Muungano wa Machi 14 ambao unasaidiwa na nchi za Magharibi. Nayla Tueni anasema wazi kwamba ingekuwa baba yake bado yu hai, asingefikiria kupigania uchaguzi.
Lakini kushinda kiti cha ubunge kwa mara ya kwanza kwa mwanamke sio jambo la uhakika, licha ya kwamba mwanamke huyo kuwa na maingiliano mazuri na familia yake. Gilberte Zwein aliyaona machungu hayo mwaka 1996 na 2000 pale aliposhindwa katika wilaya yake ya Keserwan. Baadae alichaguliwa mwaka 2005, na hivi sasa anawania tena kama mtetezi pekee wa kike, akiungwa mkono na Chama cha Free Patriotic Movement. Ukoo wa kisiasa wa Zwein unakwenda nyuma hadi babu wa Gilberte, ambaye aliwahi kuwa mjumbe wa bunge la kwanza la Lebanon pale nchi hiyo iliopapata uhuru mwaka 1943. Hamu ya Gilberte katika siasa ilianza katika ujana wake pale aliposimamia kampeni ya baba yake kuwania ubunge.
Kweli jina la familia ni shuruti muhimu ya kufanikiwa, lakini peke yake shuruti hiyo haitoshi. Kuwa tu binti wa mtu fulani haina maana utachaguliwa. Hivi sasa watu wanawapigia kura zaidi na zaidi watetezi walio na programu za kisiasa zilizo wazi. Gilberte Zwein amekuwa akijitahidi kuona wanawake zaidi wanashiriki katika siasa za Lebanon.
Vizuwizi vya kisheria huenda sio wazi wazi vinawawekea guu wanawake kufika bungeni, lakini desturi za kijamii zinaweka vizingiti ambavyo, kihistoria, vimepunguza mafanikio ya wanawake hao. Jamii ya Lebanon sio ilioelemea zaidi katika nguvu za mwanamke; wanaume wanaonekana kuwa ni muhimu zaidi kuliko wanawake bungeni.
Katika uchaguzi wa mwaka huu ambao ni ushindani baina ya upinzani unaoongozwa na Chama cha Hizbullah dhidi ya wingi unaotawala na unaoungwa mkono na nchi za Magharibi, wengi wa watetezi wa kike ni wanaojitegemea, hawaungwi mkono na kundi lolote. Kwa mfano, Bibi Therese Rizkallah, anayepigania moja kati ya viti vitatu vilivotengwa kwa ajili ya Wakristo wa madhehebu ya Maronite katika eneo la Baabda, anasema amekabiliana na malalamiko makali kutoka kwa wanaume na wanawake kutoka pande zote mbili za siasa za Lebanon. Yeye aliwahi kuwa kanali katika jeshi la Lebanon, na anauliza ikiwa wanawake wanaweza kupigana kama wanaume, kwanini wasiweze kuiwakilisha nchi yao? Bibi Rizkallah anasema huenda hana nafasi katika uchaguzi wa mara hii. lakini ikiwa hata atapata kura 100, hiyo ina maana ameonesha tafauti. Anasema akishindwa mara hii, atapigania tena mwaka 2013.