1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

LAPPEERANTA:Iran yatahadharishwa na Umoja wa Ulaya

1 Septemba 2006
https://p.dw.com/p/CDG6

Umoja wa Ulaya watahadharisha leo hii dhidi ya kupitisha uamuzi na mapema wa kuiwekea Iran vikwazo vya kiuchumi na venginevyo na kusema kwamba kwa Umoja wa Ulaya diplomasia inaendelea kubakia kuwa njia nambari moja ya kupiga hatua mbele.

Waziri wa mambo ya nje wa Finland Erkki Toumioja ambaye nchi yake inashikilia Urais wa Umoja wa Ulaya amewaambia waandishi wa habari kabla ya mkutano usio rasmi wa mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya kwamba huu sio wakati au mahala kwa jumuiya ya kimataifa kuiadhibu Iran na vikwazo kutokana na mpango wake wa kurutubisha uranium.

Katika mkutano wao huo wa siku mbili unaofanyika katika mji wa Finland karibu na mpaka wa Russia mawaziri hao wa Umoja wa Ulaya wanatarajiwa kutafuta mazungumzo mapya na Iran licha ya shinikizo la Marekani la kutaka kuchukuwa hatua mara moja ya kuiwekea vikwazo nchi hiyo.

Wizara ya mambo ya nje ya Russia imesema vikwazo vya aina yoyote ile havitopelekea kutatuliwa kwa mzozo huo.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Iran Hamid Reza Asefi amesema Jamhuri ya Kiislam ya Iran inaamini kwa njia pekee inayowezekana kufanikisha matokeo ya haki na yanayokubalika na pande zote ni kwa kupitia mazungumzo na kwa kuheshimu haki za kisheria za Iran.

Rais Mahmoud Ahmedinejad wa Iran amekuwa akirudia mara kwa mara kwamba nchi yake haitokubali kuachana na haki yake yoyote ile ya nuklea.

Mataifa ya magharibi yanaituhumu Iran kwa kutaka kutengeneza mabomu ya nuklea dai ambalo linakanushwa na Iran kwa kusema kwamba dhamira yake ni kuzalisha umeme.