1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

LAPPEENRANTA : Umoja wa Ulaya waipa Iran wiki mbili

2 Septemba 2006
https://p.dw.com/p/CDFt

Mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya wamekubaliana leo hii kuipa Iran wiki mbili zaidi kubaininisha msimamo wake juu ya kusitisha urutubishaji wa uranium baada ya serikali ya Iran kupuuza tarehe ya mwisho iliowekwa na Umoja wa Mataifa kufanya hivyo.

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Javier Solana atakutana na msuluhishi mkuu wa masuala ya nuklea wa Iran Ali Larijani wiki ijayo kujaribu kubainisha utata uliomo kwenye jibu la kurasa 21 la Iran kwa mapendekezo ya vifuta jasho vya kiuchumi na kisiasa vya mataifa makubwa iwapo nchi hiyo itakubali kusitisha shughuli zake za nuklea wanazotilia mashaka kwamba ni kwa ajili ya kutengeneza mabomu ya nuklea.

Waziri wa mambo ya nje wa Slovenia Dimitrij Rupel ameliambia shirika la habari la Uingereza Reuters baada ya mawaziri hao 25 kujadili suala hilo katika mkutano wao nchini Finland kwamba wamempa Solana wiki mbili kwa mazungumzo ya kutaka bainisho na Iran.

Akizungumza kabla ya mkutano huo wa mwaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank- Walter Steinmeir ameitaka Iran kuonesha ishara kwamba iko makini juu ya mazungumzo hayo na kwamba hawataki kufunga mlango wa mazungumzo lakini wanahitaji ishara kutoka Iran kuwa inaelekea kwenye mwelekeo wao.