1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

LAGOS: Maofisa wa Nigeria wanasema hakuna manusura katika ajali ya ndege

24 Oktoba 2005
https://p.dw.com/p/CEOz

Maofisa nchini Nigeria wametangaza kwamba hakuna aliyenusurika katika ajali ya ndege iliyotokea nchini humo jana jioni. Ripoti hii inatofautiana na ile iliyotolewa hapo awali na vyombo vya habari kwamba nusu ya watu wote 117 waliokuwa katika ndege hiyo walinusurika.

Ndege hiyo aina ya Boeng 737 ya shirika la ndege la Bellair, ilianguka magharibi mwa mji wa Lagos mda mfupi baada ya kupaa angani. Kilichoisababisha ajali hiyo bado hakijajulikana na vifaa vya kunasia sauti vya ndege hiyo bado havijapatikana.

Imeripotiwa kwamba kati ya waliokuwa ndani ya ndege hiyo ni maofisa wa ngazi ya juu wa Nigeria na jumuiya ya uchumi ya mataifa ya Afrika Magharibi, ECOWAS. Mtayarishaji wa vipindi vya televisheni kuhusu uchumi wa Afrika Kusini, Adele Lorenzo, ni miongoni mwa waliofariki dunia katika ajali hiyo.

Rais wa Afrika Kusini Thabo Mbeki amemtumia risala za rambirambi rais wa Nigeria, Olusegun Obasanjo, kufuatia kifo cha mkewe, Stella, na ajali hiyo ya ndege.