1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
HistoriaUjerumani

Kutoka Kaiser Wilhelm Spitze hadi Kilele cha Uhuru

21 Desemba 2023

Ukoloni wa Ulaya barani Afrika ulidumu kwa zaidi ya miaka 70, ambapo jamii nyingi ziliharibiwa au utambulisho wao kuchafuliwa, na hiyo ilikuwa hatua ya mwisho ya wakoloni kuifanya Afrika kuwa miliki yao.

https://p.dw.com/p/4aSZK
Mfululizo wa Makala za Kivuli cha Ukoloni wa Ujerumani zinatayarishwa na DW, shirika la kimataifa la utangazaji la Ujerumani kwa ufadhili wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani (AA). Ushauri wa mambo ya historia umetolewa na Profesa Lily Mafela, Profesa Kwame Osei Kwarteng na Reginald Kirey.
Mfululizo wa Makala za Kivuli cha Ukoloni wa Ujerumani zinatayarishwa na DW, shirika la kimataifa la utangazaji la Ujerumani kwa ufadhili wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani (AA). Ushauri wa mambo ya historia umetolewa na Profesa Lily Mafela, Profesa Kwame Osei Kwarteng na Reginald Kirey.Picha: Comic Republic

Mkasa wa Mlima Kilimanjaro

Wachagga wameishi kwenye miinuko ya mlima huo maarufu kabisa barani Afrika kwa karne nyingi. Wanakiita kilele chake Kibo.

Lakini kwa sehemu kubwa ya historia ya sasa, watoto wa Kitanzania wamefundishwa kwamba Mlima Kilimanjaro uligunduliwa mwaka 1848 na mmishionari wa Kijerumani aitwaye Johannes Rebmann.

Soma zaidi: Mauaji ya kwanza ya kimbari ya karne ya 20 Namibia

Mwanajiografia wa Kijerumani, Hans Meyer, alikibadilisha jina kilele cha mlima huo kutoka Kibo na kuwa Kilele cha Kaiser Wilhelm alipofika kilele hicho mwaka 1889.

Kivuli cha Ukoloni wa Ujerumani

Umuhimu wa Kilimanjaro kwa utamaduni wa Wachagga ulipuuzwa kabisa. Na bado, wavumbuzi wa Ulaya walikuwa wanajuwa sana maana ya kuyapa majina mapya maeneo hayo muhimu: kwamba wao walikuwa ndio mabwana wapya wa Afrika, na walikuwapo barani humo "kuwastaarabisha" wenyeji.

Matokeo yake, majina ya kienyeji yalishushwa thamani - na wakati mwengine kusahauliwa kabisa.

Soma zaidi: Uporaji wa ardhi: Kuzaliwa kwa Himaya ya Ukoloni wa Ujerumani

Ndiyo maana wakati wa kuadhimisha kuzaliwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 1964, Kilele cha Kaiser Wilhelm kwenye Mlima Kilimanjaro kilibadilishwa jina na kuitwa Kilele cha Uhuru.

Bado hadi leo kwenye Bonde la Ufa la Afrika Mashariki, Ziwa Victoria linaendelea kuitwa kwa jina hilo la mtawala wa Kiingereza wa karne ya 19.

Kivuli cha ukoloni wa Ujerumani - Sehemu ya Kwanza

Namibia, lililokuwa koloni pekee la walowezi wa Kijerumani, bado hadi leo ina majina chungu nzima ya Kijerumani.

Soma zaidi: Pambana! Jinsi Waafrika Mashariki walivyokabiliana na ukandamizaji wa kikoloni

Miongoni mwao ni mji wa Lüderitz uliopewa jina la Mjerumani wa kwanza kununuwa sehemu kubwa ya ardhi na kuanzisha mamlaka za kikoloni kwenye eneo hilo.

Hata hivyo, katika miaka ya hivi karibuni kumekuwapo juhudi za kuubadilisha jina mji huo.

Maana mbaya ya "Lebensraum"

Wanajiografia wa Ujerumani wa wakati huo, kama vile  Friedrich Ratzel, walishawishi fikra za kikoloni kwa kupendekeza kwamba Ujerumani, ikiwa kama 'taifa imara' ilikuwa na haki ya kujitanuwa kwenye yale yaliyoitwa 'mataifa dhaifu." Itikadi ya "Lebensraum", ama eneo la kuishi, ilitumika kuhalalisha ukoloni wa Kijerumani, na nchi zilizotekwa zilifanywa ziendane na utamaduni wa Kijerumani.

Kivuli cha Ukoloni wa Ujerumani - Sehemu ya Pili

"Lebensraum" ndiyo baadaye iliyokuja kuwa msingi wa fikra ya Unazi. 

Soma zaidi: Kampuni ya Woermann ilivyousafirisha ukoloni wa Ujerumani

Kuwavua watu utambulisho wao, hata baada ya maisha yao kuharibiwa kwa ukandamizaji na mateso ya ukoloni, ilikuwa hatua muhimu kwenye kuanzisha udhibiti kamili.

Vipi wakoloni wametukuzwa?

Imekuwa ni changamoto na imekuwa ikichukuliwa kwa njia tafauti.

Kumbukumbu ya ukatili wa Hermann von Wissmann katika Afrika Mashariki.

Mwanzoni mwa miaka ya 1900, mabeberu wa Kijerumani walimuita "Muafrika Mkubwa Kabisa wa Ujerumani".

Kivuli cha Ukoloni wa Ujerumani - Utwaaji wa ardhi

Mwaka 1905, sanamu lake liliwekwa mjini Dar es Salaam, na katika mji mkuu Berlin na kwengineko, mitaa ilipewa majina yake.

Soma zaidi: DW yazindua makala mpya za "Kivuli cha Ukoloni wa Ujerumani"

Lakini wa Waafrika Mashariki, Wissmann alikuwa mtu katili, na wanajeshi wake walijulikana kwa ugaidi na mauaji, uvamizi na mateso dhidi ya wenyeji.

Mnamo mwaka 1921, sanamu la Wissmann liliondoshwa na wakoloni wa Kiingereza kabla ya kujitokeza tena mjini Hamburg katikati ya karne ya 20.

Kizazi kipya cha wanafunzi wa Kijerumani walilivunja sanamu hilo mwaka 1967, wakipinga kutukuzwa ubeberu wa Ujerumani.

Kwa nini makumbusho za Ujerumani zina mabaki mengi ya binaadamu kutoka Afrika?

Yumkini msumari mmoto mkali zaidi kwa Watanzania ni suala la mali zilizoibwa na mabaki ya binaadamu kutoka Afrika Mashariki na kupelekwa Ujerumani kama ngawira za vita na kwa ajili ya utafiti wa sayansi ya ubaguzi wa rangi.

Mamia ya mafuvu ya Waafrika yalichukuwa kutoka kwenye nyanja za vita, au yaliibiwa kutoka kwenye makaburi na kupelekwa Ujerumani ambako yalioneshwa wkenye makumbusho ama kuchukuliwa na watu binafsi.

Hamilton Naki: Mvumbuzi katika kivuli cha ubaguzi wa rangi

Ni mabaki machache tu kati ya haya ndiyo yameweza kurejeshwa nyumbani kuzikwa rasmi kwa mujibu wa mila za wenyeji.

Kwa muda mrefu sasa, wanahistoria wa Kitanzania na ndugu wa wale waliouawa wakati wa ukoloni wamekuwa wakitaka mabaki hayo ya binaadamu kurejeshwa.

Na japokuwa kunaweza kukawa na kumbukumbu chache zilizoandikwa kuzungumzia kipindi cha ukoloni kwa mtazamo wa Kitanzania, simulizi za historia ya ukoloni wa Kijerumani bado zinaendelea kurithishwa vizazi kwa vizazi.

Mnamo mwezi Novemba 2023, Rais Frank Walter Steinmeier wa Ujerumani aliwatembelea Watanzania mkoani Songea kuomba msamaha kwa ukatili wa Wajerumani kwenye Vita vya Maji Maji, uliopoteza maisha ya Waafrika baina ya 120,000 na 300,000.

Alisema Ujerumani inalishughulikia suala la kuyarejesha mabaki ya miili hiyo kule yanakostahiki - kwa ndugu zao.


Mfululizo wa Makala za Kivuli cha Ukoloni wa Ujerumani zinatayarishwa na DW, shirika la kimataifa la utangazaji la Ujerumani kwa ufadhili wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani (AA). Ushauri wa mambo ya historia umetolewa na Profesa Lily Mafela, Profesa Kwame Osei Kwarteng na Reginald Kirey.