1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ongezeko la watu Nigeria: Njia ya umaskini au ustawi?

14 Julai 2023

Makadirio ya Umoja wa Mataifa yameonyesha kuwa jumla ya idadi ya watu nchini Nigeria, itaongezeka maradufu kutoka milioni 200 hadi zaidi ya milioni 401 ifikapo mwisho wa mwaka 2050.

https://p.dw.com/p/4TvND
Symbolbild I Hunger in der Welt noch groß
Picha: Sun Ruibo/Unicef/Photoshot/picture alliance

Ikiwa hali hiyo haitadhibitiwa, idadi ya watu nchini humo itazidi na kufikia milioni 728 ifikapo mwaka 2100. Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia watoto UNICEF, limeeleza kuwa Nigeria ina idadi ya zaidi ya vijana milioni 65 wenye umri wa miaka 10-24. Vijana hao wanaoingia katika umri wa uzazi, watasababisha idadi ya watu kuongezeka zaidi.

Mtaalamu wa demografia katika Chuo Kikuu cha Lagos, John Oyefara ameiambia DW kwamba, wanaona ongezeko la watu linaweza kuwa rasilimali kwa nchi, lakini matatizo yanayokwamisha maendeleo ikiwemo umaskini mkubwa, utawala mbovu na ukosefu wa utulivu wa kisiasa, yataongezeka iwapo ongezeko la watu litaendelea kutodhibitiwa.

Uhaba wa rasilimali ukilinganisha na idadi ya watu.

Mtaalamu huyo ameongeza kusema rasilimali zilizopo haziwezi kukidhi mahitaji ya kimsingi ya idadi ya watu inayoongezeka, huku akiiangazia ripoti iliyotolewa na benki ya dunia iliyobainisha hali mbaya zaidi kwa vijana inayooesha ukosefu wa ajira nchini Nigeria umeongezeka kutoka 6.4% mwaka 2010 hadi 33.3% mwishoni mwa 2020. Hali hiyo pia imesababisha kuwepo uhaba wa vifaa katika sekta ya afya, usalama wa chakula, makazi na usafiri.

Joseph Blabo ambae ni mwananchi wa kawaida alipoongea na DW amesema ilikuwa vigumu kwake kuwa na watoto wengi kwa wakati mmoja kwa sababu ingemuwia ugumu kutengenezea maisha yao bora ya baadaye. Na amekua akiangalia hali ya nchi, jinsi uchumi unavyozidi kuwa mbaya siku hadi siku, amejiona alifanya uamuzi mzuri kwa kutotaka kuwa na watoto wengi. Mawazo hayo ya Joseph ni tofauti tofauti na bwana Sani Umaru, mwenye wake watatu na watoto 18. Ambae ameieleza DW mtazamo wake wa kuwa na familia kubwa ni baraka kutoka kwa Mungu.

Onyo la kuchukuliwa hatua za dharura kudhibiti ongezeko la watu.

Nae Mkurugenzi wa Kituo cha Afrika Magharibi cha Mabadiliko Endelevu ya Vijijini,  Michael Ayamga amesema, Nigeria inahitaji kuchukua hatua za dharura za kudhibiti masuala ya uzazi ambapo ameeleza kwa sasa kiwango cha uzazi cha wanawake wa Nigeria ni watoto 5.1, kinyume na kiwango cha kimataifa cha wastani wa uzazi ambacho ni 2.4 kwa kila mwanamke. Pia ameeleza inatakiwa kuanza kuongeza nguvu kwenye elimu ya uzazi wa mpango sambamba na kudhibiti kiwango kinachoendelea kwa sasa.

Ayamga ameiambia DW, ana matumaini zaidi kwa siku zijazo, mradi masharti fulani yatimizwe, huku akizitolea mfano China na India kuwa ni nchi za kuigwa na Afrika, zilizowekeza katika kuelimisha watu. amesema Nigeria inahitaji kufuata mfano wa China na India wa kutengeneza mazingira ambayo yanawaruhusu vijana kujifunza ili kufanikiwa. Ameeleza ni lazima umakini uwe katika kuelekeza upya mitaala ya elimu na kubadilisha mfumo wa kutoa mafunzo yanayofaa kwa siku zijazo.

Soma zaidi:Rais wa Nigeria akabidhiwa mikoba ya ECOWAS

Ayamga amesema "India na China ziliendeleza uwezo wa vijana katika teknolojia na katika maeneo mengine ambayo yanahusisha teknolojia. Kisha wakaanza kutoa ujuzi huo kwa mamlaka nyingine zilizowahitaji, na hiki ndicho haswa kinachohitajika inapaswa kugeuza idadi ya watu kuwa mtaji.

Chanzo: DW