1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Ugaidi

Kundi la Dola la kiislamu ladai kufanya shambulizi Kabul

Josephat Charo
10 Januari 2024

Kundi linalojiita Dola la Kiislamu IS limedai kuhusika na mlipuko ulioilenga gari moja mashariki mwa mji wa Kabul ambao umewaua watu angalau watatu.

https://p.dw.com/p/4b3Gh
Afghanistan | mlipuko mjini Kabul
Kundi la IS limetangaza uadui dhidi ya watawala wa Taliban nchini Afghnaistan.Picha: Wakil Kohsar/AFP/Getty Images

Kundi linalojiita Dola la Kiislamu IS limedai kuhusika na mlipuko ulioilenga gari moja mashariki mwa mji wa Kabul ambao umewaua watu angalau watatu katika shambulizi la pili la kundi hilo lililosababisha vifo nchini Afghanistan katika kipindi cha wiki moja.

Msemaji wa jeshi la polisi mjini Kabul Khali Zadran amesema watu watatu waliuliwa na watu wengine wanne kujeruhiwa na bomu lililokuwa limefichwa kwenye mkokoteni karibu na basi dogo mashariki mwa Kabul jana Jumanne.

Soma pia: Kundi la IS nchini Afghanistan ladai kuhusika na shambulizi la bomu nchini Pakistan ambalo liliwauwa watu 54.

Zadran ameliambia shirika la habari la Ufaransa AFP kwamba polisi imemtia mbaroni na inamzuilia mshukiwa mmoja aliyekiri kuhusika na shambulizi hilo.

Kundi la Dola la Kiislamu limedai kuhusika na hujuma hiyo katika taarifa yake kwenye mtandao wa Telegram likisema limelipua kilipuzi kwenye gari lililokuwa likiwasafirisha wafanyakazi wa gereza la Pul-e-Charki.