1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kufikia mwaka 2100 tutakuwa watu bilioni 9 duniani

Ibrahim Swaibu
20 Julai 2020

Utafiti mpya umebaini kuwa ifikapo mwaka 2100, idadi ya watu kote ulimwenguni itakuwa ni watu bilioni 8.8. Makadirio hayo yaliyochapishwa Julai 15 katika Jarida la "The Lancet” ni chini kwa takribani watu bilioni 2.

https://p.dw.com/p/3fbaM
Eid Shopping in Asien Indonesien Bekasi
Picha: AFP/Rezas

Kulingana na makadirio ya Umoja wa Mataifa ifikapo mwaka 2030 idadi ya watu duniani itakuwa bilioni 8.5, watu bilioni 9.7 katika mwaka 2050 na mnamo mwaka wa 2100, Umoja huo unakadiria kuwa idadi ya watu duniani kote itapindukia bilioni 10.9.

Hata hivyo utafiti wa hivi karibuni uliofanyika na Taasisi ya hesabu pamoja na tathmini ya afya katika Chuo Kikuu cha Washington Marekani (IHME), umebaini kuwa ifikapo mwishoni mwa karne hii idadi ya watu kote duniani itakuwa bilioni 8.8.

Utafiti huo umebaini kuwa wakati viwango vya uzazi vikizidi kupungua na kwa upande mwingine makadirio ya kuishi yakipanda, idadi ya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano itashuka kwa asilimia 40. Hii ikimaanisha idadi hiyo kushuka kutoka watoto milioni 681 mnamo mwaka 2017 hadi watoto milioni 401 ifikapo mwaka 2100.

Kwa mujibu wa utafiti huo pia ifikapo mwishoni mwa karne hii ya 21, mataifa 183 kati ya 195 ambayo yanapinga mmiminiko wa wakimbizi, yatakuwa chini ya kiwango kinachotakiwa ili kuweza kundeleza idadi ya watu katika mataifa hayo.

Utafiti huo uliochapishwa Julai 15 katika Jarida la Kimataifa la afya "The Lancet” umebaini kuwa idadi ya watu itashuka kwa nusu katika zaidi ya nchi 20 ikiwemo Japan, Spain, Italia, Thailand, Ureno, Korea Kusini pamoja na Poland. Kadhalika katika miaka 80 ijayo, idadi ya watu nchini China itashuka kutoka watu bilioni 1.4 kwa sasa hadi watu milioni 730.

England Strand in Bournemouth
Umati wa watu katika fukwe ya Bournemouth UingerezaPicha: picture-alliance/empics/A. Matthews

Hata hivyo utafiti huo umeonesha kuwa katika Kusini mwa jangwa la Afrika, idadi ya watu itaongezeka mara tatu, Nigeria ikitajariwa kuwa na idadi ya watu milioni 800 katika mwaka 2100, na kuwa katika nafasi ya pili yenye watu wengi zaidi duniani baada ya India ambayo inakadiriwa kuwa itakuwa na watu bilioni 1.1 ifikapo mwaka 2100.

Christopher Murray, mkurugenzi mtendaji wa Taasisi iliofanya utafiti huo ameliambia shirika la habari la AFP kuwa makadirio hayo ambayo ni chini kwa takribani watu bilioni 2 ikilinganishwa na yale ya Umoja wa Mataifa, yanatoa ishara nzuri kwa mazingiria kutokana na kutozishinikiza mifumo ya uzalishaji chakula pamoja na kwamba itatoa nafasi za ajira katika mataifa ya Kusini mwa jangwa la Sahara.

Aidha utafiti huo umeeleza kuwa huenda chumi za mataifa yaliyoko nje ya bara la Afrika yakaathirika kutokana na kupungua kwa nguvu kazi pamoja na wengi wa raia wake kuwa na umri mkubwa wa kustaafu. Ifikapo mwaka 2100, Idadi ya watu walio na zaidi ya miaka 65 itakuwa bilioni 2.37, hiyo ikiwa ni zaidi ya theluthi ya watu wote duniani. Wakati huo huo, idadi ya watu wenye zaidi ya miaka 80 itapanda kutoka milioni 140 hadi kufikia milioni 866. Utafiti umeongeza.

Kama suluhisho ya kuendeleza kiwango cha idadi ya watu katika mataifa yaliondelea, watafiti wamependekeza mataifa hayo kuweka sera rafiki kuhusu uhamiaji pamoja na kutoa misaada kwa watu wanaotaka kuza watoto.