1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Korea Kaskazini yafyatua kombora kuelekea Mashariki

5 Januari 2022

Korea Kusini na Japan zinasema Korea Kaskazini imefyatua kile kinachoonekana kuwa kombora la masafa marefu kuelekea baharini. Hili ndilo kombora la kwanza la aina hiyo kufyatuliwa na Korea Kaskazini mwaka 2022.

https://p.dw.com/p/45AKe
USA | Abschuss unscharfen Trident II Rakete
Picha: U.S. Navy/ZUMA/picture alliance

Kulingana na  taarifa ya muungano wa wanadhimu wakuu katika jeshi la Korea Kusini, kombora hilo lilirushwa katika bahari mashariki mwa rasi ya Korea na baraza la usalama la Korea Kusini limeelezea wasiwasi wake kuhusiana na jaribio hilo. 

Rais wa Korea Kusini Moon Jae In amethibitisha kuwa Korea Kaskazini imefanya jaribio hilo la kombora na kuna hofu kwamba hii italeta mvutano na kuharibu zaidi mahusiano ya Korea hizi mbili.

Moon lakini ameshauri kuwa yanayotokea hayapaswi kuwakatisha tamaa ya mazungumzo ili kupata suluhu ya pamoja.

soma zaidi:Korea Kaskazini yafanya jaribio la kombora kwa kutumia nyambizi

Kikosi cha ulinzi wa pwani cha Japan kimesema kwenye taarifa yake mapema leo kwamba kombora hilo huenda likawa ni kombora la masafa marefu.

Korea Kaskazini inakabiliwa na vikwazo vya kimataifa kutokana na tabia zake za kujaribisha makombora lakini imeendeleza vitendo hivyo mara kwa mara.

Jaribio hilo linafanyika siku kadhaa baada ya kiongozi wa taifa hilo Kim Jong Un wiki iliyopita kuapa kuendelea kujiimarisha kijeshi.