1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Korea Kaskazini yaendelea na vitisho vyake

MjahidA5 Aprili 2013

Korea Kaskazini imehamisha makombora mengine kwenye mwambao wake wa Mashariki tayari kwa mashambulizi dhidi ya Marekani, huku nchi hiyo inayotishiwa kushambuliwa ikisema inachukua tahadhari kutokana na vitisho hivyo.

https://p.dw.com/p/18ARn
Jeshi la Korea Kaskazini
Jeshi la Korea KaskaziniPicha: picture-alliance/dpa

Kulingana na chombo cha habari cha Yonhap cha Korea Kaskazini kikimnukuu afisa mmoja wa serikali nchini humo, makombora mawili tayari yameshasafirishwa kwa treni mapema wiki hii na kuwekwa katika magari tayari kwa kushambulia.

Kwa upande wake Wizara ya ulinzi ambayo ilithibitisha kupelekwa kwa kombora la kwanza ilikataa kutoa maoni yake juu ya habari za hivi karibuni kwamba makombora mengine yamesafirishwa Mashariki mwa pwani ya nchi hiyo.

Hata hivyo afisa mmoja wa jeshi amekiambia chombo hicho cha Yonhap kwamba, makombora yaliyosafirishwa yametegeshwa Mashariki na Magharibi mwa pwani ya Korea Kaskazini.

Rais wa Korea kaskazini Kim Jong Un akiwa pamoja na maafisa wake wa jeshi
Rais wa Korea kaskazini Kim Jong Un akiwa pamoja na maafisa wake wa jeshiPicha: picture-alliance/dpa

Vitisho hivyo vya Korea kaskazini ni mojawapo ya misururu ya vitisho vya wiki kadhaa sasa, kufuatia vikwazo vya Umoja Wa Mataifa dhidi yake na mazoezi ya pamoja ya kijeshi kati ya Marekani na Korea kusini.

Marekani yatoa maoni yake

Huku hayo yakiarifiwa Marekani imesema itaweka mizinga ya kujikinga na makombora katika kisiwa chake cha Pasifiki cha Guam kuimarisha uwepo wake wa kijeshi katika eneo hilo.

Hata hivyo wachambuzi wengi wanaofuatilia swala hili kwa makini wanasema Korea Kaskazini haina uwezo wa kuishambulia Marekani.

Waziri wa ulinzi wa Marekani, Chuck Hagel, amesema vitisho vinavyotolewa na Pyongyang vinatia hofu kwa taifa hilo zima na hata washirika wake kama Korea Kusini na Japan.

Waziri wa ulinzi wa Marekani Chuck Hagel
Waziri wa ulinzi wa Marekani Chuck HagelPicha: REUTERS

Tangu vitisho kuanza kutolewa kumekuwa na fununu kwamba mashambulizi hayo huenda yakafanyika siku ya kuzaliwa kwa kiongozi wa zamani wa nchi hiyo, hayati Kim Il-Sung, ambayo ni katikati ya mwezi wa Aprili.

Ban Ki Moon aisihi Korea Kaskazini kusimamisha vitisho

Vitisho hivyo vya mara kwa mara kutoka Korea Kaskazini kwa Marekani vimezua hisia mbali mbali miongoni mwa jamii ya kimataifa.

Kwa upande wake katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, akisema kwamba vitisho vya aina hiyo vinatia hofu na huenda vikasababisha athari kubwa.

Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon
Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki MoonPicha: AFP/Getty Images

"Nadhani wamekwenda mbali katika vitisho vyao, na nina wasi wasi kwamba iwapo ghasia hizo zitatokea katika rasi ya Korea basi swala hili litakuwa na athari kubwa sana," Alisema Ban Ki Moon.

Hapo jana Korea kaskazini iliwazuia wafanyikazi kutoka Korea kusini kuingia katika kiwanda cha Keosong. Hatua hiyo inalenga kuwasimamisha kazi wafanyakazi takriban 53,000 kutoka Korea Kusini.

Mwandishi Amina Abubakar/AFP

Mhariri Josephat Charo