1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaKorea Kusini

Korea Kaskazini kupanua mazoezi yake ya kijeshi

7 Februari 2023

Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un ameahidi kupanua mazoezi ya kijeshi na kuimarisha utayari wa nchi hiyo kwa vita wakati taifa hilo likijiandaa kwa maadhimisho ya siku ya kuundwa kwa jeshi lake.

https://p.dw.com/p/4NBAY
Militärparade in Nordkorea
Picha: KCNA/dpa/picture alliance

Shirika la KCNA limeripoti kuwa Kim alioongoza mkutano huo wa baraza kuu la kijeshi la chama cha wafanyakazi kilichoko madarakani ambapo maafisa wake walijadiliana kuhusu majukumu makubwa ya kijeshi na kisiasa kwa mwaka huu na masuala ya muda mrefu yanayohusu mwelekeo wa uimarishaji wa jeshi. KCNA imeongeza kusema kuwa baadhi ya masuala yaliyojadiliwa ni suala la kupanua na kuimarisha operesheni na kukabiliana na mazoezi ya jeshi la watu wa Korea KPA kukabiliana na hali iliyoko na zaidi kujiandaa kikamilifu kwa vita.

Picha zaonesha wanajeshi wa Korea Kaskazini wakifanya mazoezi

Picha za satelaiti za kibiashara zimeonyesha wanajeshi wa Korea Kaskazini wakifanya mazoezi mjini Pyongyang, huku Korea Kusini ikisema kuwa inafuatilia ongezeko la shughuli zinazohusiana na matukio hayo. Mkutano huo wa kijeshi pia unafuatia hatua ya Korea Kaskazini siku ya Alhamisi ya kushtumu mazoezi ya kijeshi yaliyofanywa na Marekani na washirika wake na kusema wamefikia kiwango cha hatari na kutishia kuigeuza rasi hiyo kuwa uwanja mkubwa wa vita vikali.

Deutschland | Konferenz zum Ukraine-Krieg in Ramstein
Lloyd Austin - Waziri wa ulinzi wa MarekaniPicha: Michael Probst/AP Photo/picture alliance

Katika taarifa siku ya Alhamisi, wizara ya mambo ya nje ya Korea Kaskazini, ililaani ziara ya waziri wa ulinzi wa Marekani Lloyd Austin nchini Korea Kusini na kusema taifa lake halihitaji mazungumzo wakati Marekani inafuatilia sera za uhasama. Korea Kusini na Marekani zimeungana kuimarisha mazoezi ya pamoja ya kijeshi kufuatia mwaka wa kuvunjwa kwa vikwazo vya majaribio ya silaha yaliyofanywa na Korea Kaskazini na kuikasirisha nchi hiyo ambayo inachukulia mazoezi hayo kuwa ya uvamizi.

Marekani na Korea Kusini zafanya mazoezi ya pamoja ya kijeshi

Wiki iliyopita, washirika hao wa kiusalama walifanya mazoezi ya pamoja ya kijeshi ya anga yaliohusisha mabomu ya kimkakati na ndege za kivita na kuilazimu Korea Kaskazini kuonya kuwa mazoezi kama hayo huenda yakachochea vita kamili. Mazoezi hayo ya pamoja ambayo ni ya kwanza mwaka huu, yanakuja siku moja baada ya Lloyd Austin na mwenzake wa Korea Kusini, kuapa kuimarisha ushirikiano wa kiuslama kukabiliana na Korea Kaskazini inayozidi kujiimarisha kwa silaha za nyuklia. Siku ya Jumatatu, wizara ya ulinzi ya Korea Kusini, ilisema kuwa mwishoni mwa juma, Puto la Korea Kaskazini lilivuka hadi kwenye anga yake, lakini halikuwa na tishio. Shirika la habari la Yonhap liliwanukuu maafisa wakisema kuwa puto hilo liliaminika kuwa la hali ya hewa na kwamba wizara hiyo imechukuwa hatua bila ya kutoa maelezo zaidi.