1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kony akutana na waandishi wa habari kwa mara ya kwanza.

8 Agosti 2006

Kwa kiongozi wa waasi ambae hadhi yake ni karibu na jambo la kubuni kuliko binadamu halisi katika eneo alikozaliwa la kaskazini mwa Uganda, Joseph Kony alikuwa anaonekana mwenye wasi wasi mkubwa.

https://p.dw.com/p/CBId

Hii ilikuwa hata hivyo , mkutano wake wa kwanza ana kwa ana na waandishi wa habari.

Akifunikwa na hali isiyofahamika tangu alipoanzisha mapambano yake miaka 20 iliyopita, muonekano wa Kony umekuwa ukitafsiriwa kwa wastani moja kwa moja katika masuala ya mauaji, kuwakatakata watu viungo na kuwakamata watoto na wanawake suala ambalo limekuwa likifanywa na wapiganaji wake wa Lord’s Resistance Army.

Yeye alikuwa kimya kabisa, haonekani, na kusababisha baadhi ya watu kujiuliza iwapo Kony ni mtu anayeishi ama ni mawazo tu ya watu.

Wakitambua kuwa mahusiano na jamii halikuwa suala muhimu kwa kiongozi wao, waasi hao wanajaribu kila wawezavyo hivi sasa kutengeneza picha ya kiongozi wao kuwa ni mkombozi katika mazungumzo ya amani na serikali ya Uganda ambayo yamekuwa yakiendelea katika mji mkuu wa jimbo la kusini wa Juba tangu mwezi wa Julai.

Akiwa anatakiwa na mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita kuhusiana na mashtaka ya uhalifu wa kivita, hakuna mtu ambaye alitarajia kuwa Kony atatokea hadharani.

Lakini wiki iliyopita , Kony mwenye umri wa miaka 43 akivalia shati jeupe la mikono mifupi na suruali, na viatu vyeusi , alitoka katika maficho yake msituni katika mpaka wa jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo na Sudan tayari kukutana na waandishi wa habari.

Ilikuwa sio yale aliyoyasema ambayo yalikuwa ya kusisimua lakini alivyoonekana . Macho makali , anayeonekana kushtushwa, na mwenye hali ya wasi wasi , Kony anaonekana kuwa hana wasi wasi akiwa msituni kuliko kukabiliana na waandishi wa habari wenye kamera.

Kwa waandishi wa habari ambao wametumwa kupata habari kutoka kwake, kujitokeza kwake kumekuwa ni zawadi ya kungoja kwa muda wa wiki nzima.

Wakijiunga na msafara wa amani wa kiasi watu 200 waliokwenda katika mpaka wa Sudan na Kongo, ambako waasi hao sasa wanamakao yao , waandishi wa habari walipanda ndege ya mizigo chapa Antonov mjini Juba kabla ya kutua katika uwanja wa ndege wa Maridi na kusafiri kwa saa tisa kwa gari hadi katika kituo hicho cha waasi cha Nabanga.

Siku zilikatika wakati waandishi hao wakiishi katika kijiji cha nyumba za nyasi, wakati wakiomba kupata mahojiano nae.

Waliweza kualikwa katika bunge la LRA, katika banda la nyasi, na ambapo inabidi kutembea kwa muda wa saa nzima katika msitu wa Kongo, ambako waliweza kupata kwa mara ya kwanza kumuona Kony.

Akiwasalimu wajumbe wa serikali ya Uganda kwa kushikana nao mkono na tabasamu , akiwa amevalia nguo za kijeshi za kijani na kofia, kamanda huyo alikuwa anaonekana hana wasi wasi kabisa katika maeneo yake aliyoyazowea.

Licha ya sifa yao ya kuogopesha, wanajeshi vijana wadogo wa jeshi la Kony hawakuweza kujizuwia kutabasamu wakati wakijikusanya mbele ya wapiga picha na kuchukuliwa picha za kamera.

Walionekana kuwa wakakamavu ghafla wakati kiongozi wao hatimaye alipojitokeza kutoka msituni kukutana na wapatanishi kabla ya kukaa chini katika kiti cha plastiki na kutoa taarifa fupi.

Mimi ni mtu, mimi ni binadamu, mimi ni Joseph Kony, alisema, huku akiwa hatulii kitini wakati kamera zinafyatuliwa kuchukua picha. Yale maneno ambayo watu wanasema kwangu ni propaganda, wanachafua jina langu , ili watu wasinipende kama binadamu.

Niligeuka kutoa taarifa ya wito wake wa kusitisha mapigano katika simu yangu. Mara nilipogeuka kuangalia tena , amekwisha potea, amerejea katika msitu alisema mwandishi mmoja wa habari.