1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAfrika

Kongo yawazika watu 200 waliouwawa vitani na M23

2 Septemba 2024

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imefanya mazishi ya miili ya watu 200 waliofariki dunia katika mazingira ya aina mbalimbali kwenye makambi ya wakimbizi wa ndani karibu na mji wa Goma.

https://p.dw.com/p/4kC8M
Raia wa Kongo wakiwa katika moja ya kambi ya wakimbizi
Raia wa Kongo wakiwa katika moja ya kambi ya wakimbiziPicha: Moses Sawasawa/AP/picture alliance

 Maombolezo yalifanyika kwenye uwanja wa michezo mjini Goma ambapo viongozi mbalimbali kutoka serikali kuu walishiriki. Watu hao ni wale waliofariki tangu kuzuka kwa vurugu baina ya jeshi la Kongo na waasi wa M23 miaka minne iliyopita kwenye eneo hilo.

Imekuwa ni siku ya huzuni sana hapa mjini Goma ambapo shughuli zilisimama mchana kutwa wa leo Jumatatu.

Maelfu ya raia walikuja kushiriki hafla hii ya kuwapa heshima za mwisho watu hao 200 waliofariki baada ya kukimbia ghasia katika vijiji vyao miaka michache iliyopita.

Ndugu wa waathirika na ambao bado wanaendelea kuhangaika katika makambi ya wakimbizi karibu na mji wa Goma wamelinyooshea kidole cha lawama kundi la wapiganaji wa M23 kuwa chanzo cha vifo hivyo. Jeanne NSIMIRE ni mke aliyempoteza mumewe:

Soma pia:Kwanini usitishaji vita Mashariki ya Kongo hauheshimiwi?

Wakati maiti zikipewa heshima zao za mwisho na viongozi kutoka serikali kuu ya Kinshasa kwenye uwanja wa michezo katikati mwa mji wa Goma, ndugu wengine wamelaani ukimya wa jumuiya ya kimataifa kwa kulifumbia macho swala la usalama mashariki ya Kongo.

Gavana wa kijeshi wa mkoa wa Kivu Kaskazini, Peter Chirimwami, ni miongoni mwa mwa viongozi walioshiriki hafla hii ya mazishi na kutoa mkono wa pole kwa waathiriwa wa mauaji aliyosema yanafanywa na waasi wa M23 mashariki mwa Kongo.

Miili yazikwa Nyiragongo

Baada ya hafla hiyo, miili ilizikwa katika eneo la Nyiragongo kwenye makaburi ya  kumbukumbu kwa wahanga wote wa vita vya M23 yaliyotengwa maalum na serikali.

Radio, chombo cha kueneza amani Kongo

Tukio hili linakuja miezi minne baada ya wakimbizi wa ndani 35 kuuawa kwa bomu katika kambi moja karibu na mji wa Goma, mnamo tarehe 3 ya mwezi Mei mwaka huu.

Soma pia:M23 wachukua udhibiti wa sehemu kubwa ya Rutshuru

Ripoti zinasema kuwa zaidi ya raia milioni sita wameyakimbia makaazi yao na kupatiwa hifadhi ndani ya makambi ya wakambizi ambamo hali ya kiutu inaendelea kuwa mbaya kila kukicha.