1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kongo yaituhumu M23 na Rwanda kuhujumu usafiri wa anga

30 Julai 2024

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo imewatuhumu waasi wa kundi la M23 na vikosi vya Rwanda vinavyowaunga mkono kuvuruga shughuli za usafiri wa anga kwenye mkoa wa Kivu Kaskazini.

https://p.dw.com/p/4ispC
Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo | Goma
Hali mashariki mwa Kongo.Picha: picture alliance / ASSOCIATED PRESS

Imesema wanafanya hivyo kwa kuingilia mfumo wa mawasiliano unaotumia teknolojia ya GPS. Katika taarifa yake iliyotolewa usiku wa kuamkia leo, serikali ya Kongo imesema ilifanya uchunguzi kubaini chanzo cha hitilafu kwenye mfumo wa mawasiliano ya kuongoza ndege unaotumia teknolojia ya GPS baada ya ripoti za kuwepo mparaganyiko.

Taarifa hiyo imesema uchunguzi wake umegundua vikosi vya jeshi la Rwanda ndiyo vimehusika kusababisha hitilafu hiyo kwa kuhujumu mfumo uliopo. Imesema vikosi hivyo vimekuwa vikituma mawimbi tofauti ya mawasiliano ya GPS kwa dhamira ya kuvuruga ule uliopo.

Kongo imeonya kuwa vitendo hivyo vinahatarisha usalama wa usafiri wa anga na kuziweka rehani juhudi za kiutu zinazotegemea usafiri huo kupeleka misaada kwa maelfu ya watu waliokimbia mapigano.