1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kongamano la "Loya Jirga" lafunguliwa Afghanistan

Oumilkheir Hamidou
29 Aprili 2019

Malefu ya wajumbe kutoka kila pembe ya Afghanistan wanaanza kongamano kuu "Loya Jirga", mjini Kabul kuzungumzia juhudi za Marekani za kufikia makubaliano ya amani pamoja na Wataliban. Hatua za usalama zimeimarishwa.

https://p.dw.com/p/3HdD9
Afghanistan Peace Talks Afghanistan Loya Jirga Kabul Ashraf Ghani
Picha: picture-alliance/AP Photo/R. Gul

Zaidi ya wanasiasa 3000, wakuu wa kidini, viongozi wa makundi ya kikabila na wanachama wengine wa mashirika ya kijamii wanahudhuria mkutano huo wa siku nne unaotajwa kuwa muhimu zaidi katika historia ya hivi karibuni ya Afghanistan.

"Tunabidi tufafanue mwongozo wa majadiliano yetu pamoja na wataliban" amesema rais wa Afghanistan Ashraf Ghani alipokuwa anaufungua mkutano huo."Tunataka ushauri thabiti kutoka kwenu," amesisitiza.

 "Loya Jirga " au Kongamano kuu, kama linavyoitwa kwa lugha ya pashtun, linapewa umuhimu mkubwa nchini Afghanistan. Kongamano hilo huitishwa baadhi ya wakati ikihitajika ili kusaka maridhiano kuhusu mada muhimu za kisiasa..

Loya Jirga ya mwaka huu inafanyika katika wakati ambapo wamarekani na wataliban wanajadiliana tangu miezi kadhaa sasa kuhusu uwezekano wa kuondolewa wanajeshi wa Marekani ili badala yake wataliban wakubali  miongoni mwa mengineyo, kuweka chini silaha .

Viongozi wa Afghanistan wanaotajwa na waasi kuwa "vikaragosi wa Washington", hawakuwa wakijumuishwa katika mazungumzo hayo. Duru nyengine za mazungumzo kati ya wataliban na Marekani itafanyika mnamo siku zinazokuja nchini Qatar.

Rais Ashraf Ghani akifungua kongamano la Loya Jirga mjini Kabul
Rais Ashraf Ghani akifungua kongamano la Loya Jirga mjini KabulPicha: Reuters/O. Sobhani

Rais Ghani anatuhumiwa kutaka kuitumia Loya Jirga kwa masilahi yake ya kisiasa

Serikali ya Ashraf Ghani inataraji kongamano hilo la  Loya Jirga litafafanua masharti ya Kabul kuweza kufikia makubaliano, ikiwa ni pamoja na kuheshimiwa katiba iliyoko, kulindwa haki za wanawake, kuheshimiwa uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa mtu kutoa maoni yake.

Hata hivyo, Rais Ghani binafsi haungwi mkono na wote. Mkuu wa baraza tendaji, Abdullah Abdullah, kiongozi wa zamani wa kivita Gulbuddin Hekmatyar na mshauri wa zamani wa usalama wa taifa Mohammad Haneef Atmar wanasusia kongamano hilo. Wanalalamika wakisema limeandaliwa bila ya kushauriwa na kutumiwa na Ashraf Ghani ili kufanya kampeni kwa ajili ya uchaguzi wa rais Septemba mwaka huu.

Rais Ghani aliwaalika pia wataliban washiriki katika kongamano hilo. Lakini waasi hao wanaoendesha vita vya chini kwa chini tangu mwaka 2001, wamesusia mwaliko huo.

Katika taarifa waliochapisha wiki iliyopita, walionya uamuzi wowote au azimio litakalopitishwa katika kongamano hilo la Loya jirga "halitakubaliwa na watoto wa kweli wanaojitolea kwaajili ya nchi yao."

Hatua za usalama zimeimarishwa mjini Kabul ambako sehemu kubwa ya shughuli zimesita  na njia zinazoelekea milimani kufungwa. Wiki nzima hii imetangazwa kuwa wiki ya mapum ziko ili kuhakikisha usalama mjini Kabul.

 

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/AP/AFP

Mhariri: Mohammed Khelef