1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kondom za Baba Mtakatifu na Urusi kwenye NATO zangonga vichwa

Abdu Said Mtullya22 Novemba 2010

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wasema kauli ya Baba Mtakatifu juu ya matumizi ya kondom ni muhimu

https://p.dw.com/p/QF9m
Baba Mtakatifu Benedikt wa 16 alegeza msimamo wa kanisa juu ya matumizi ya kondom.Picha: AP

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wanatoa maoni yao juu ya kauli iliyotolewa na Baba Mtakatifu Benedikt wa 16 juu ya matumizi ya kondom.

Mhariri wa gazeti la Westfalenblatt anasema kauli ya Baba Mtakatifu imeleta matumaini japo mtu angelipenda kumwona Baba Mtakatifu akipiga hatua ndefu zaidi katika juhudi za kupambana na maradhi ya ukimwi.Mhariri wa gazeti la Nürnberger anakumbusha kwamba ni Baba Mtakatifu huyo huyo aliesema mwaka jana tu, kwamba matumizi ya kondom yatalifanya tatizo la ukimwi liwe kubwa zaidi. Lakini sasa kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki duniani amefanya mageuzi.

Hata hivyo mhariri wa Sächsiche anasema mtu hawezi kutumai kumwona Baba Mtakatifu akileta mabadiliko makubwa mnamo kipindi cha muda mfupi. Mhariri huyo anaeleza kuwa ni wazi Baba Mtakatifu hawezi kuruhusu matumizi ya kondom leo, na kesho tu awaruhusu makasisi wafunge ndoa na kesho kutwa atoe ridhaa ili wanawake wawe makasisi! Lakini sauti ya chini chini aliyoitumia katika kuwasilisha ujumbe juu ya kondom imeonyesha kuwa kiongozi huyo wa wakatoliki duniani anatumia njia ya busara katika kuleta mabadiliko.

Na mhariri wa Berliner Zeitung anasema Baba Mtakatifu amepiga hatua muhimu, lakini hajaleta mapinduzi ndani ya kanisa. Mhariri huyo anauliza? Je, Baba Mtakatifu pia anaruhusu matumizi ya kondom ili kuzuia ujauzito miongoni mwa wasichana, na jee anaruhusu matumizi ya kondom ili kudhibiti idadi ya watoto.? Anachosema Baba Mtakatifu ni kwamba, kondom zinaweza kutumika katika mazingira fulani. Kwa hiyo hakuna mapinduzi yaliyofanyika. Baba Mtakatifu bado ameng'ang'ania dunia yake ile ile ya hapo awali.

Gazeti la Volksstimme linazungumzia juu ya ukurusa mpya wa uhusiano uliofunguliwa baina ya Jumuiya ya Kijeshi ya NATO na Urusi. Mhariri wa gazeti hilo, anatilia maanani msimamo wa nchi za NATO wa kuizingatia Urusi kuwa mshirika mwenye haki sawa. Anasema ni muhimu kutambuaa hayo, kwani katika enzi za vita baridi, Urusi ilikuwa adui wa NATO.

Uamuzi wa viongozi wa NATO kutilia maanani hofu na matarijio ya Urusi, ndiyo msingi wa kujenga uhusiano wa kuaminiana katika sekta za kijeshi, kiuchumi na kisiasa baina ya pande mbili hizo.

Mwandishi: Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen/

Mhariri: Othman Miraj/