1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Klabu ya Al Nassr ya Saudi Arabia yamsaini Cristiano Ronaldo

31 Desemba 2022

Cristiano Ronaldo amejiunga na klabu ya Saudi Arabia ya Al Nassr jana Ijumaa katika uhamisho ambao huenda ukabadili soka katika ukanda wa mashariki ya kati.

https://p.dw.com/p/4LapX
Saudi Arabien Cristiano Ronaldo vor Wechsel zu Al Nasssr
Picha: Frank Hoermann/SVEN SIMON/picture alliance

Ronaldo amejiunga na klabu hiyo ya Saudi Arabia kwa mkataba utakaodumu hadi angalau mwaka 2025.

Klabu ya Al Nassr iliweka picha kwenye mitandao ya kijamii ikimuonyesha Ronaldo, ambaye ni mshindi mara tano wa tuzo ya mchezaji bora duniani Ballon d'or, akiwa ameshikilia jezi ya timu hiyo, huku Al Nassr ikipongeza usajili huo na kuuita historia.

Uhamisho huo pia unampa nafasi Ronaldo mwenye umri wa miaka 37 kutia kibindoni mshahara mkubwa kuelekea kukamilika kwa maisha yake ya soka la kulipwa.

Ripoti za vyombo vya habari zimedai kuwa nyota huyo wa Ureno atapokea mshahara wa hadi dola milioni 200 kwa mwaka akiichezea Al Nassr.

Nahodha huyo wa Ureno alikuwa ni mchezaji huru baada ya kuondoka Manchester United kufuatia mahojiano yenye utata aliyofanyiwa na mtangazaji Piers Morgan ambapo aliikosoa klabu hiyo ya Old Trafford.

Mshambuliaji huyo amesema "ana hamu ya kupata uzoefu wa kucheza katika ligi nyengine ya kandanda na katika nchi tofauti."

Lakini licha ya usajili wa Ronaldo kutazamiwa kupiga jeki soka la Mashariki ya Kati, kutatochea mjadala juu ya serikali ya Saudi Arabia kutumia michezo kama njia ya kuboresha sifa zake kimataifa.

Klabu ya Newcastle United inayoshiriki ligi kuu ya Premia ilinunuliwa na Saudi Arabia kupitia mfuko wake wa uwekezaji wa umma, na utawala huo wa kifalme unanuia kutuma ombi la kuandaa michuano ya Kombe la Dunia la FIFA mwaka 2030.