1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiongozi wa zamani wa Kijeshi wa Guinea atoroshwa gerezani

Angela Mdungu
4 Novemba 2023

Watu wenye silaha wamevamia gereza kuu mjini Conakry na kumtorosha kiongozi wa zamani wa kijeshi wa Guinea Moussa Dadis Camara.

https://p.dw.com/p/4YP3A
Moussa Dadis Camara
Moussa Dadis CamaraPicha: Schalk van Zuydam/AP/picture alliance

Kufuatia tukio hilo, Waziri wa Sheria wa Guinea, Charles Alphonse Wright ametangaza kufungwa kwa mipaka ya nchi hiyo. Taarifa ya waziri huyo imetolewa saa chache baada ya kuibuka kwa mapambano ya risasi katika eneo la Kaloum mjini Conakry.

Kwa mujibu wa Wright, Camara alitoroka gerezani sambamba na watu wengine wawili. Moussa Dadis Camara aliyeingia madarakani mwaka 2008 kwa mapinduzi ya kijeshi amekuwa kizuizini akihusishwa na mauaji ya mwaka 2009.

Soma zaidi: Guinea yakumbuka mauaji ya 2009

Mauaji hayo yalifanyika wakati wanajeshi wake walipowafyatulia risasi watu waliokuwa wakifanya maandamano ya amani kupinga nia yake ya kugombea Urais, baada ya mapinduzi yaliyomuweka madarakani. Makundi ya haki za binadamu yanasema watu wasiopungua 157 walikufa katika tukio hilo.