1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiongozi wa wapiganaji ashitakiwa ICC kwa uhalifu Darfur

5 Aprili 2022

Kesi ya kwanza ya uhalifu wa kivita katika jimbo la Darfur imeanza siku ya Jumanne katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita ya ICC mjini The Hague nchini Uholanzi.

https://p.dw.com/p/49V7Q
Niederlande, Den Haag | Prozess gegen Ali Kushayb wegen Kriegsverbrechen in Darfur
Picha: International Criminal Court/AA/picture alliance

Mahakama hiyo imesema kiongozi wa zamani wa kundi la wapiganaji nchini Sudan Ali Muhammad Ali Abd-Al-Rahman, aliongoza kampeni ya mauaji, ubakaji na mateso kote katika jimbo la Darfur. Mshirika huyo wa zamani wa kiongozi aliyeondolewa madarakani nchini Sudan Omar al-Bashir, anakabiliwa na mashitaka 31 ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinaadamu kutokana na jukumu lake katika mzozo huo zaidi ya miaka 20 iliyopita.

Kesi yake ndio ya kwanza mbele ya mahakama hiyo ya ICC kwa uhalifu uliofanywa Darfur, ambapo zaidi ya watu 300,000 waliuawa na wengine milioni mbili na nusu wakiyahama makazi yao kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa.

Niederlande, Den Haag | Prozess gegen Ali Kushayb wegen Kriegsverbrechen in Darfur
Ali Muhammad Ali Abd-Al-Rahman akiwa mahakamani ICCPicha: International Criminal Court/Handout/AA/picture alliance

Abd-Al-Rahman anayejulikana kama Ali Kushayb na mwenye umri wa miaka 72, alikuwa kamanda mwandamizi wa kundi la Janjaweed, kundi hatari la wapiganaji lililoundwa na serikali ya Sudan, alikanusha mashitaka hayo wakati kesi hiyo ya kihistoria ilipofunguliwa.

Kesi hiyo ya ICC ni ya kukabiliana na ukatili uliofanywa na vikosi vya serikali ya Sudan katika eneo la Darfur karibu miongo miwili iliyopita. Kesi hiyo ilifunguliwa huku kukiwa na malalamiko ya kimataifa kwa ukatili unaoshutumiwa

vikosi vya Urusi katika vita vya Ukraine na ni ukumbusho kwamba Mahakama za kimataifa zinaweza kuwawajibisha watuhumiwa wa uhalifu hata kama mchakato wenyewe unaweza kuwa mrefu wenye kusuasua.

Mwendesha mashtaka Karim Khan aliita kesi hiyo  kuwa "wakati muhimu wa kujaribu kuiamsha amani kutoka katika usingizi wake na kujaribu kuihamasisha kwa vitendo."