1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Kiongozi wa upinzani Urusi ahukumiwa miaka 25 jela

17 Aprili 2023

Mahakama moja nchini Urusi siku ya Jumatatu imemhukumu kifungo cha miaka 25 gerezani moja ya wanasiasa wakuu wa upinzani nchini humo, Vladimir Kara-Murza, Jr.

https://p.dw.com/p/4QCuY
Mwanasiasa wa upinzani Vladimir Kara-Murza
Vladimir Kara-Murza akisikiliza hukumu yake mbele ya mahakama mjini Moscow.Picha: Moscow City Court press service/AFP

Kwa mujibu wa shirika la habari la Associated Press Vladimir Kara-Murza, Jr ametiwa hatia kwa makosa ya uhaini baada ya kupinga hadharani uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

Hukumu yake ni ishara ya wazi ya juhudi za ikulu ya Kremlin yakuwafunga midomo wakosoaji wote wa vita vyake nchini Ukraine.

Vladimir Kara-Murza, Jr, mwanaharakati wa kisiasa na mwandishi wa habari ambaye amenusurika majaribio miwili ya kuuwawa kwa kupewa sumu na anaodai kuwa watawala wa Urusi, anayapinga madai dhidi yake na ameyataja kuwa adhabu kwa msimamo wake wa kumkabili rais Vladimir Putin.

Ameifananisha kesi na hukumu dhidi yake mfano wa mashauri yaliyokuwa yakiendeshwa enzi ya kiongozi wa zamani wa Dola ya Kisovieti, Josef Stani.

Makundi ya Haki za Binadamu na serikali za magharibi zimelaani vikali hukumu dhidi ya mwanasiasa huyo na kuzitaka mamlaka za Urusi kumwachia huru Vladimir Kara-Murza, Jr.

Shirika la kutetea Haki za Binadamu la Amnesty International limemtangaza mwanaharakati huyo kuwa mfungwa wa kisiasa.

Matamshi ya ukosoaji kuhusu vita vya Ukraine ndiyo chimbuko la yote 

Mapigano nchini Ukraine
Urusi imekuwa ikitumia njia mbalimbali kuwakandamiza wote wanakosoa uvamizi wake nchini Ukraine.Picha: Ukrainian Presidential Chief of Staff Andriy Yermak/AFP

Mashtaka dhidi ya Kara-Murza, aliye na uraia pacha wa Urusi na Uingereza na ambaye amekuwa rumande tangu kukamatwa kwake mwaka mmoja uliopita, yametokana na hotuba yake aliyoitoa mwezi Machi mwaka 2022 mbele ya Baraza la Wawakilishi la Jimbo la Arizona huko Marekani ambapo alikosoa uvamizi wa Ukraine. Inasadikika alitoa hotuba nyingine kama hizo sehemu mbali mbali dunaini.

Siku chache baada ya Urusi kuivamia Ukraine, mamlaka mjini Mosocw zilipitisha sheria inayofanya kuwa hatia kwa mtu kusambaza kile kinatajwa kuwa "habari za uongo” kuhusu jeshi.

Watawala wa Urusi wamekuwa wakitumia sheria hiyo kudhibiti ukosoaji wa kile Kremlin inakitaja kuwa "operesheni maalum ya kijeshi” nchini Ukraine.

Kupitia hotuba fupi aliyoitoa baada ya hukumu yake, Kara-Murza amesema amehukumiwa kwenda jela kwa sababu ya kazi ya "miaka mingi ya kuukabili udikteta wa Putin”, ukosoaji wake kwa vita nchini Ukraine na juhudi zake za muda mrefu za kuhimiza vikwazo vikali vya nchi za magharibi dhidi ya maafisa wa Urusi wanaohusishwa na ukiukaji wa Haki za Binadamu.

"Ninafahamu kuwa siku inakuja ambapo giza lililotanda nchini mwetu litapotea”, baba huyo wa Watoto watatu aliiambia mahakama kupitia ujumbe uliotumwa kwenye mtandao wa Twitter. "Siku hiyo itafika kama ilivyo lazima kwa msimu wa machipuko kuwasili hata baada ya msimu wa baridi kali”

Kara-Murza alikuwa mtulivu wakati wote hukumu yake ilipokuwa ikisomwa. Baadaye wakili wake alikaririwa akisema Kara-Murza amweleza : "Thamani yangu imepanda; nimebaini kwamba nimefanya kila kitu kwa usahihi kabisa. Miaka 25 ni gharama ninayovuna kwa kufanya nilichofana na kuamini katika hilo, kama raia, mzalendo na mwanasiasa”

Ukosoaji wahanikiza hukumu dhidi ya mwanasiasa huyo 

Hukumu dhidi ya Kara-Murza imezusha ukosoaji kutoka mashirika na asasi chungunzima za kutetea haki za binadamu.

Asasi iitwayo Memorial, miongoni mwa asasi kongwe kabisa za kutetea haki za binadamu nchini Urusi, zimemuorodhesha Kara-Murza kama mfungwa wa kisiasa kama ilivyofanywa na Amnesty International.

Russland | Aktivist Vladimir Kara-Murza auf der "foreign agent" Liste
Picha: Sergei Bobylev/TASS/picture alliance/dpa

Serikali za Uingereza, Marekani, Ujerumani na nyingine upande wa magharibi zimekosoa kwa matamshi makali hukumu hiyo.

"Vladimir Kara-Murza amepinga uvamizi wa Urusi nchini Ukraine kwa ushujaa mkubwa kwamba kilichofanyika kilikuwa ni ukiukwaji usio mfano wa sheria za kimataifa na mkataba wa Umoja wa Mataifa” amesema Waziri wa mambo ya kigeni wa Uingereza katika taarifa iliyotolewa na ofisi yake.

Wizara yake imesema imemwita Balozi wa Urusi mjini London kulalamika kuhusiana na hukumu hiyo.

Wizara ya mambo ya nchi za nje ya Marekani imemsifu Kara-Murza pamoja na wanasiasa wengine wa upinzani walio gerezani kwa kusimama imara kutete haki za binadamu na misingi ya uhuru.

Pia imerejea wito wake wa kutaka Urusi iwaachie huru zaidi ya wafungwa 400 ikiwemo Kara-Murza walihukumiwa kwa sababu za kisiasa.