1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiongozi wa upinzani Israel apewa jukumu la kuunda serikali

Saleh Mwanamilongo
6 Mei 2021

Kiongozi wa upinzani Israel, Yair Lapid amepewa jukumu la kuunda serikali, baada ya waziri mkuu mkongwe Netanyahu kushindwa kuunda serikali ya muungano.

https://p.dw.com/p/3t2UE
Parlamentswahlen in Israel I Yesh Atid
Picha: Ilia Yefimovich/dpa/picture alliance

Hatua hiyo inafuatia mashauriano na viongozi wa vyama kuamua kama mbunge yeyote alikuwa na njia ya kuunda muungano unaoweza kuiwekea kikomo enzi isiyo ya kawaida ya mkwamo wa kisiasa. Lapid, mtangazaji wa zamani wa televisheni wa siasa za wastani, alisema Israel inaumia, baada ya mkwamo wa kisiasa wa miaka miwili, na kuwa atalenga kuumaliza muhula wa Netanyahu wenye mgawanyiko, kwa kuunda serikali ya umoja ambayo itadhihirisha kuwa Waisrael hawachukiani.

Changamoto za Lapid

Kiongozi wa upinzani Yair Lapid kuunda serikali ya muungano nchini Isreal.
Kiongozi wa upinzani Yair Lapid kuunda serikali ya muungano nchini Isreal.Picha: Tania Krämer/DW

Uteuzi wa Lapid umefuatia mazungumzo baina ya rais Rivlin na Naftali Bennett wa chama cha Yamina, Yair Lapid wa chama cha Yesh Atid na vilevile wajumbe wa vyama vingine vyenye uwakilishi bungeni. Chama cha Yair Lapid kilichukua nafasi ya pili katika uchaguzi uliopita. Rais Rivlin amesema kuwa uteuzi huo utachangia kumaliza mkwamo wa kisiasa.

''Lapid ana fursa ya kuunda serikali na kupata uungwaji mkono wa Knesset, japokuwa changamoto ni nyingi.''

 Rais Rivlin alifahamisha nia yake ya kuweko na mbunge mwingine anayeweza kuteuliwa kuwa waziri mkuu, katika makubaliano ya ugawanaji madaraka kwa mzunguuko. Awali, yair Lapid alisema kuwa lipendekeza jina la Naftali Bennet kwa wadhifa huo wa Waziri MKuu. Benjamin Netanyahu aliuta muungano huo kuwa athari kwa Israel.

''Ni ukweli wa wazi kwamba itakuwa ni serikali ya mrengo wa kushoto ambayo ni mchanganyiko wa ukosefu wa mtazamo, isiyo na ushindani na isiyo na uwajibikaji''',alisema Nentanyahu

Chama cha Likud cha Benjamin Netanyahou, kilichukuwa nafasi ya kwanza kwenye uchaguzi wa mwezi Machi 23. Hali iliomuezesha Netanyahou kupewa muda wa siku 28 wa kutafuta maelewano ya kuunda serikali mpya ya Israel lakini muda huo umemalizika usiku wa kuamkia jana Jumatano bila ya kupatikana mafanikio.

Mwisho wa enzi ya Netanyahu ?

Benjamin Nentanyahu,waziri Mkuu anayeondoka nchini Isreal.
Benjamin Nentanyahu,waziri Mkuu anayeondoka nchini Isreal.Picha: Ronen Zvulun/REUTERS

Kushindwa kwa Netanyahou kuunda serikali ya mseto kunadhihirisha mpasuko mkubwa wa kisiasa uliopo nchini Israel. Wapiga kura waligawanyika hadi kuwapigia kura wagombea wa vyama vya Kiyahudi vya mrengo wa kulia na chama cha kiislamu cha wahafidhina.

Vizingiti vingi vilivyosababisha Netanyahu kushindwa kuunda serikali ya mseto na vyama vilivyokuwa na uwezekano wa kuunda naye serikali hiyo ni matatizo ya kisheria yanayomkabili.

Aidha, kura ya maoni iliotolewa Jumatano na taasisi ya Kidemokrasia nchini Isreal inaonyesha kuwa asilimia 70 ya raia wa Israel wanadhani kuwa mazungumzo kwa ajili ya kuunda serikali ya mseto hayatofaulu na uchaguzi mpya unatarajiwa kuitishwa.