1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaHaiti

Kiongozi wa Haiti atua Puerto Rico njiani kurudi nyumbani

6 Machi 2024

Waziri Mkuu wa Haiti anayekabiliwa na shinikizo Ariel Henry, amewasili kwenye kisiwa cha Puerto Rico usiku wa kuamkia leo akijaribu kurejea nyumbani katikati mwa mzozo na magenge ya wahalifu yanayomtaka kujiuzulu.

https://p.dw.com/p/4dCtA
Waziri Mkuu wa Haiti, Ariel Henry.
Waziri Mkuu wa Haiti, Ariel Henry.Picha: Richard Pierrin/AFP

Duru zinasema ndege ya Henry ilitua kwenye mji mkuu wa Puerto Rico, San Juan, na kufichua mahali aliko kiongozi huyo tangu alipoonekana mara ya mwisho akiwa ziarani nchini Kenya wiki iliyopita.

Haijafahamika ni vipi Henry atarejea nchini Haiti katika wakati makundi ya watu wenye silaha yameapa kumzuia kuingia nchini humo yakisema yanamtaka ajiuzulu.

Tangu alipoondoka Haiti wiki iliyopita kwa ziara ya kusaka uungaji mkono wa kimataifa ili kurejesha utulivu nchini mwake, makundi ya wahalifu yamefanya mfululizo wa mashambulizi yaliyoutikisa mji mkuu Port-au-Prince.

Hapo jana yalikishambulia chuo cha mafunzo ya polisi siku moja baada ya kujaribu kuchukua udhibiti wa uwanja mkuu wa ndege nchini humo.