1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiongozi wa #BringBackOurGirls kuwania urais Nigeria

10 Oktoba 2018

Oby Ezekwesili ni mwanamama jasiri na maarufu nchini Nigeria anayetaka hivi sasa kupambana katika ulingo wa siasa za kuwania urais katika taifa ambalo kwa miaka mingi ni wanaume ndio wanaozihodhi siasa za nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/36J9v
Initiative Bringbackourgirls Nigeria
Picha: DW/K. Gänsler

Mwanamke aliyeongoza kampeni ya kimataifa ya kutaka waachiwe huru wasichana washule ya Chibok waliotekwa nyara na kundi la itikadi kali la Boko Haram sasa ameamua kugombea urais nchini Nigeria.Oby Ezekwesili ni mwanamke mashuhuri nchini humo.

Oby Ezekwesili ni mwanamama jasiri na maarufu nchini Nigeria anayetaka hivi sasa kupambana katika ulingo wa siasa za kuwania urais katika taifa ambalo kwa miaka mingi ni wanaume ndio wanaozihodhi siasa za nchi hiyo.

Aliwahi kuwa makamu wa rais wa benki kuu ya dunia na pia ni mwasisi mwenza wa shirika la kimataifa la Transparency ambalo liko mstari wa mbele katika kuipiga vita rushwa duniani,ambayo kwahakika ndio tatizo kubwa katika nchi yakeo hiyo yenye utajiri wa mafuta,Nigeria.

Nigeria Abuja Proteste BBOG
Picha: DW/U. Musa

Lakini pengine anafahamika zaidi hasa katika mapambano yake ya kupigania kuachiwa huru wasichana wa shule waliokuwa wametekwa nyara na kundi la wanamgambo wa Boko Haram linalotumia kisingizio cha dini ya kiislamu kuendeleza uovu na ukatili. Kundi hilo liliwateka nyara wasichana zaidi ya 200 wa shule kutoka jamii ya wachibok mwaka 2014.

Kampeini aliyoianzisha bibi Ezekwesili iliungwa mkono hata na aliyekuwa mke wa rais wa zamani wa Marekani,Michelle Obama pamoja na viongozi wengi mashuhuri ambao waliishinikiza bila kuchoka serikali ya Nigeria kutia msukumo wa kuachiwa huru watoto hao wa kike.

Ikumbukwe kwamba polisi iliwahi hata kuyavunja kwa kutumia nguvu  baadhi ya maandamano ya kampeini hiyo ya Bring Back our Girls  lakini baada ya kufanyika mazungumzo kwa muda,iliripotiwa kwamba mamilioni ya dolla yalitolewa na kupewa kundi la Boko Haram kama kigombozi kilichosababisha kuachiwa huru  wasichana chungunzima mwaka jana.

Buhari BBOGs
Picha: Getty Images/Afp/P. Ojisua

Lakini mpaka wakati huu zaidi ya wasichana 100 hawajarudi majumbani kwao lakini kama haitoshi kisa kingine cha kutekwa nyara wasichana kikatokea tena mapema mwanzoni mwaka huu.

Rais Mohammadu Buhari aliyetoa ahadi ya kupambana na Boko Harama pamoja na rushwa alipoingia madarakani 2015 serikali yake ilijitapa kuwa mshindi katika kisa hicho cha kuachiwa huru wasichana wa Chibok dhidi ya Boko Haram.

Sasa lakini bibi Ezekwesili anataka kupambana na rais huyo mwenye umri wa miaka 75 na anampa changamoto  hasa kuhusiana na ahadi alizozitowa rais huyo katika kampeini zake. Mapambano hayo ni kuelekea uchaguzi wa rais Februari mwaka 2019.

Lakini tatizo kubwa  Nigeria ni ule mtizamo uliopo kuelekea wagombea wanawake na hasa kwakuwa raia wengi nchini humo wanahisi mwanamke mahala pake ni jikoni.Na hata rais Buhari mwenye aliwahi kusema akiwa amesimama pembeni ya mwanamke mwenye nguvu duniani Kansela Angela Merkel wa Ujerumani kwamba yeye ana maarifa makubwa kuliko mkewe ambaye anafahamu mengi kuhusu jikoni,sebuleni na kwengineko.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW