1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Al Qaida yapata Pigo kwa kumpoteza kiongozi

Mjahida16 Juni 2015

Kundi la Al Qaida limethibitisha mtu wa pili katika uongozi wa kundi hilo ambaye ni mkuu wa tawi lake kubwa na lililo na nguvu nchini Yemen ameuwawa katika mashambulizi ya angani yaliyoongozwa na Marekani.

https://p.dw.com/p/1Fhsk
Kiongozi muhimu wa kundi la Al Qaida tawi la Yemen Nasir al-Wahishi
Kiongozi muhimu wa kundi la Al Qaida tawi la Yemen Nasir al-WahishiPicha: AFP/GettyImages

Hii leo kundi hilo la Alqaida limethibitisha kifo cha Nasir al-Wahishi, kupitia taarifa ya video iliotolewa na tawi la kundi hilo katika rasi ya kiarabu, iliosema tayari nafasi ya kiongozi huyo aliyewahi kufanya kazi kama msaidizi binafasi wa Osama Bin Laden imechukuliwa na naibu wake Qassim al-Raimi.

"Taifa letu la kiislamu, shujaa wetu ameondoka kuwa na mwenyezimungu, kwa jina la mwenyezi mungu damu ya waanzilishi wa kundi hili inatupa moyo zaidi wa kuendelea," alisema kiongozi mkuu wa kundi hilo Khaled Batrafi aliyeongeza kuwa vita vyao dhidi ya Marekani vitaendelea.

Kifo cha al-Wahishi ni katika msururu wa mauaji ya maafisa wa kundi hilo tawi la Yemen akiwemo kiongozi mkuu wa kijeshi Nasr al-Ansi, kiongozi wa itikadi za kidini Ibrahim al-Rubish na wengine, hivi karibuni.

Matokeo ya mashambulizi ya angani nchini Yemen
Matokeo ya mashambulizi ya angani nchini YemenPicha: Reuters/Khaled Abdullah

Al- Wahishi ni miongoni mwa wanamgambo 23 wa Alqaida waliotoroka jela moja mjini Sanaa nchini Yemen mnamo Februari mwaka 2006, na mwaka 2009 alitangaza kuundwa kwa kundi la AQAP, lililowajumuisha wanamgambo wa Yemen na Saudi Arabia.

Hata hivyo awali maafisa wa Yemen walisema shambulizi hilo la angani lililofanywa na marekani liliwauwa wanamgambo wa tatu katika eneo linalodhibitiwa na al Qaeda Kusini mwa mji wa bandari wa Mukalla wiki iliyopita. Kwa upande wake Marekani inasema bado inajaribu kuthibitisha iwapo kweli Nasir al-Wahishi ameuwawa.

Waasi wa Yemen wajiunga katika mazungumzo ya amani Geneva

Wakati huo huo ujumbe wa wanamgambo wa Yemen umewasili mjini Geneva kwa siku ya pili ya mazungumzo ya amani yanayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa baada ya ujumbe huo kukwama mjini Djibouti kwa siku moja. Kutokuwepo kwa waasi hao katika mazungumzo hayo yaliyoanza hapo jana yaliofunguliwa na Katibu Mkuu wa Umoja huo Ban Ki Moon kulizua wasiwasi juu ya mustakbal wake.

Ndege ya wanamgambo hao iliondoka mjini Sanaa siku ya Jumapili mchana lakini ikalazimika kutuwa na kusubiri Djibouti kwa saa 24. Waasi hao wanaoungwa mkono na Iran wanazishutumu Misri na Sudan kwa kutoruhusu ndege yao kusafiri katika anga zao.

Wafuasi wa wanamgambo wa Houthi wakionyesha silaha zao
Wafuasi wa wanamgambo wa Houthi wakionyesha silaha zaoPicha: Reuters/K. Abdullah

Katika mazungumzo hayo hapo jana Ban Ki Moon alizungumzia umuhimu wa kusimamishwa kwa mapigano kwa angalau wiki mbili ili kutoa nafasi ya waislamu kufunga mwezi mtukufu wa ramadhani na na kutoa misaada ya kibinaadamu kwa mamiliobni ya watu walioathirika na vita hivyo.

Mwanidhi Amina Abubakar/AP/AFP

Mhariri Mohammed Abdul-Rahman