Kinachoendelea kuhusu kuuawa mwandishi Jamal Khashoggi
22 Oktoba 2018Shirika la habari la serikali Anadolu limeripoti kwamba waendesha mashitaka kadhaa wa Uturuki waliwahoji mashahidi watano ambao ni wafanyakazi wa ubalozi huo mdogo kuhusiana na kifo cha Khashoggi. Kwa mujibu wa shirika la habari la NTV la nchini Uturuki, gari la balozi mdogo wa Saudi Arabia limepatikana katika mji wa Sultangazi ulio katika wilaya ya Istanbul. Na taarifa zinasema kuwa polisi watalichunguza gari hilo.
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ameapa kufichua ukweli wote kuhusu mauaji ya mwandishi huyo wa habari Jamal Khashoggi akisisitiza kwamba kwamba nchi yake ina wajibu wa kuueleza ulimwengu ukweli kuhusu kilichotokea. Erdogan anatarajiwa kutoa taarifa kamili kesho kuhusu kifo cha Khashoggi.
Saudi Arabia ilikiri mwishoni mwa wiki kuwa Khashoggi aliuawa katika ubalozi wake mdogo ulioko Istanbul, lakini imesema haijui ulipo mwili wake na mrithi wa mfalme wa Saudi Arabia Mohamed bin Salman amesisitiza kuwa hakufahamu juu ya operesheni ya kumuua mwandishi huyo aliyekuwa mkosoaji mkubwa wa utawala wake.
Ujerumani imezisisitizia nchi za Umoja wa Ulaya kuonyesha ushirikiano katika suala la mauzo ya silaha kwa Saudi Arabia. Kansela wa Ujerumani Angela Merkel aliwaambia waandishi wa habari mjini Berlin kwamba anaunga mkono hatua ya kusimamisha mauzo ya silaha kwa Saudi Arabia kufuatia mauaji ya mwandishi Jamal Khashoggi.
Waziri wa Uchumi wa Ujerumani Peter Altmaier, anayehusika na kuidhinisha mauzo ya silaha, aliiambia televisheni ya Ujerumani ya ZDF kwamba kwa wakati huu, hawezi kuidhinisha mauzo yoyote ya silaha kabla ya kubainika kilichotokea.
Wakati huo huo wafanya biashara wakuu na wawakilishi wa Ulaya wamejitenga na Saudi Arabia tangu sakata la kutoweka na kuuawa kwa mwandishi wa habari Jamal Khashoggi, na wengi wamesema hawatahudhuria mkutano wa uwekezaji wa wiki hii. Falme hiyo ya Kiarabu ilikuwa na matumaini kwamba mkutano huo ungelitumika kujijenga na kuongeza umaarufu wake kimataifa.
Mwandishi:Zainab Aziz/DPA/AP/AFPE/RTRE
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman