1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kim Jong Un ziarani China

19 Juni 2018

Viongozi wa China na Korea Kaskazini wakutana Bejing kuzungumzia kilichojitokeza katika mkutano wa kilele wa Singapore kati ya Kim Jong Un na Donald Trump

https://p.dw.com/p/2zrcM
China - Kim Jong Un zu Besuch bei Xi Jinping (Screenshot aus China's CCTV)
Picha: picture-alliance/AP Photo/CCTV

Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un amempa maelezo rais wa China Xi Jinping kuhusu mkutano wake wa kilele na rais wa Marekani Donald Trump. Kiongozi huyo wa Korea Kaskani amefanya ziara China  ambayo inaonesha juhudi za China katika kubakia kuwa mzizi wa diplomasia kuhusu suala la Nyuklia katika kanda hiyo.

Ziara ya Kim Jong Un China ni ya tatu tangu mwezi Machi na imekuja wakati serikali ya mjini Beijing ikijaribu kuimarisha nafasi yake kama msuluhishi kati ya Marekani na jirani huyo wa China, Korea Kaskazini. Kiongozi wa Korea Kaskazini ambaye inaaminika aliwasili katika mji mkuu wa China leo asubuhi alikutana na Xi katika ukumbi wa jamhuri ya umma wa watu wa China wa Ornate.

Alipokelewa kwa heshima kamili ya kiongozi wa nchi ikiwa ni pamoja na gwaride la kijeshi pamoja na shangwe za watoto waliomkaribisha. Kituo cha televisheni cha China CCTV kilisema kwamba kiongozi huyo wa Korea Kaskazini aliishukuru China na kuisifu kwa kuunga mkono hatua ya kuondowa silaha za Nyuklia katika rasi ya Korea na kubeba dhima muhimu ya kulinda amani na usalama wa rasi hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa,Korea Kaskazini inataraji kushirikiana na China na nchi nyingine kuunga mkono na kuanzisha utaratibu imara na thabiti wa amani utakaodumu muda mrefu katika rasi ya Korea na kuanza juhudi za pamoja za kufikia amani ya kudumu katika rasi hiyo ya Korea.

China - Kim Jong Un zu Besuch bei Xi Jinping (Screenshot aus China's CCTV)
Picha: picture-alliance/AP Photo/CCTV

Kadhalika imeelezwa katika ripoti hiyo kwamba rais Xi Jinping wa China ameitaka Korea Kaskazini na Marekani kuendelea kusimamia matokeo ya mkutano wa kilele uliofanyika baina ya viongozi hao wawili nchini Singapore Juni 12. Ikumbukwe kwamba Trump na Kim Jong Un waliahidi katika mkutano wa pamoja na waandishi habari kufanya kazi kwa pamoja kuelekea hatua ya kuondowa kabisa silaha za Nyuklia katika rasi ya Korea.

Marekani inaitegemea China katika utekelezaji wa vikwazo vya kiuchumi vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Korea Kaskazini hali ambayo inatowa uwezekano wa kuipa nguvu China katika mgogoro wake unaozidi kuongezeka wa vita vya kibiashara na Marekani. Kim alitarajiwa kuiomba China msaada katika kupunguziwa vikwazo ili Korea Kaskazini iweze kuondowa silaha zake za Nyuklia. Mtaalamu wa masuala ya uhusiano wa kimataifa kutoka chuo kikuu cha Beijing Wang Wong anasema viongozi wa Korea Kaskazini na China wako katika mashauriano kuhusu jinsi ya kuchukua hatua ya pamoja ya kulipeleka mbele suala la Nyuklia la Korea.

Kufuatia mkutano wa kilele wa Singapore China ilipendekeza kwamba baraza la usalama la Umoja wa Mataifa linaweza kufikiria kulegeza vikwazo vya kiuchumi dhidi ya mshirika wake huyo wa enzi ya  vita baridi. Kwa mujibu wa mtaalamu huyo Huenda China haikuwepo katika meza ya mazungumzo ya mkutano wa kilele Singapore lakini bado inashikilia nafasi muhimu ya kuwa na ushawishi mkubwa nyuma ya pazia. Ziara ya leo ya Kim Jong Un Beijing inaonesha kwamba China ni mshirika muhimu sana katika mazungumzo hayo ya Nyuklia ya Korea.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri:Josephat Charo

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW