1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kim Jong Un akutana na rais wa China Xi Jinping

Isaac Gamba
28 Machi 2018

Vyombo vya habari vya serikali ya China na vile vya Korea Kaskazini vimethibitisha kwamba kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un amekutana na rais wa China  Xi Jinping mjini Beijing

https://p.dw.com/p/2v74t
Kim Jong Un in China
Picha: picture-alliance/XinHua/dpa/J. Peng

Shirika la habari la China limeripoti kuwa kiongozi huyo wa Korea Kaskazini alifanya ziara ya kushtukiza nchini China wiki hii na hivyo kuhitimisha siku kadhaa za uvumi iwapo kweli Jumapili iliyopita alisafiri kwa treni kwenda China.

Ziara hiyo iliyoanza Jumapili hadi Jumatano ilikuwa ni ziara ya kwanza ya Kim Jong Un nje ya nchi  inayofahamika tangu aliposhika madaraka mwaka 2011.

Kiongozi huyo alikuwa na mazungumzo na rais wa China Xi Jinping mjini Beijing ikiwa ni pamoja na kuandaliwa karamu yeye pamoja na mkewe Ri Sol Ju.

Wakati wa ufunguzi wa karamu hiyo Kim alisema amekuwa na mazungumzo yenye mafanikio na rais Xi Jinping yanayohusu kuendeleza ushirikiano kati ya nchi hizo mbili, kuimarisha amani na uthabiti katika rasi ya Korea pamoja na masuala mengine na kuongeza kuwa aliona ni vyema yeye mwenyewe kukutana ana kwa ana kwa mazungumzo na Xi Jinping kuhusiana na mustakabali wa nchi hizo mbili na kuongeza hakuna swali la kuhoji kuhusiana na yeye kuzuru China kama ziara yake ya kwanza tangu ashike madaraka.

Vyombo vya habari vya Korea Kaskazini vimeripoti  kwamba Kim Jong Un pia amemualika rais wa China Xi Jinping kuzuru Korea Kaskazini mwaliko ambao Xi ameupokea kwa furaha.

Aidha kwa mujibu wa shirika la habari la China Xinhua Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un amemueleza rais wa China  Xi Jinping kuwa Korea Kaskazini inazingatia umuhimu wa kuondoa silaha za nyukilia na kuongeza kuwa Korea Kaskazini ina nia ya kuwa na majadiliano na Marekani pamoja  na mkutano wa kilele utakaowahusisha viongozi wa nchi hizo mbili.

 Kim Jong Un azungumzia utatuzi wa mzozo katika rasi ya Korea

Peking China Nordkorea Gespräche Xi Jinping Kim Jong Un
Kim Jong Un katika picha ya pamoja na rais wa China Xi Jinping mjini BeijingPicha: picture-alliance/Xinhua/J. Peng

Amesema suala linalohusiana na mzozo katika rasi ya Korea linaweza kutatuliwa kama Korea Kusini na Marekani zitatengeneza mazingira ya amani na uthabiti ikiwa ni pamoja na kukubaliana na juhudi zinazofanywa na Korea Kaskazini katika kutafuta suluhisho la mzozo huo.

China ni mshirika wa karibu wa Korea Kaskazini lakini mahuasiano kati ya pande hizo mbili yalionekana kuzorota baada ya China kuunga mkono vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Korea Kaskazini vinavyolenga kuibana kuhusiana na mipango yake ya silaha za nyukilia.

Wakati hayo yakiendelea ikulu ya Marekani ya White House imesema serikali ya China imefanya mawasiliano hapo jana Jumanne na Marekani kwa ajili ya kuwataarifu  maafisa wa Marekani juu ya  ziara hiyo ya kiongozi wa Korea Kaskazini nchini China.

Msemaji wa ikulu ya Marekani Sarah Huckabee Sanders alisema taarifa hiyo inahusisha ujumbe binafsi kutoka kwa rais Xi Jinping kwenda kwa rais Donald Trump.

Aidha afisa mmoja kutoka ofisi ya rais ya Korea Kusini amesema Korea Kusini pia ilikuwa inasubiri  kuhabarishwa kwa kina na China  juu ya ziara hiyo ya Kim Jong Un nchini China.

Mwandishi: Isaac Gamba/DW/AFPE

Mhariri:Josephat Charo