1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kikosi kipya cha UM na AU kwa Dafur

25 Mei 2007

Kuna mipango ya kuunda kikosi cha pamoja kati ya umoja wa Mataifa na umoja wa Afrika cha hadi askari 23,000 kwa mkoa wa Dafur,Sudan. Mashauriano yanaendelea.

https://p.dw.com/p/CHDm

Umoja wa mataifa na wa Afrika (African union) umetunga mipango ya kikosi cha kuhifadhi amani mkoani dafur,Sudan .Kikosi hicho kitajumuisha zaidi ya wanajeshi 23,000 kiingiza pia askari polisi na watumishi wengine kwa shabaha ya kuzuwia fujo .

Kikosi hicho kiitwacho “hybrid” kinabidi kwanza kuidhinishwa na Baraza la Usalama la UM na Halmashauri ya usalama ya Umoja wa Afrika unaoadhimisha leo mjini Addis Ababa,Ethiopia, miaka 44 tangu kuasisiwa OAU hapo 1963.Baadae mpango huo utafikishwa mbele ya serikali ya Sudan.

Balozi wa marekani katika UM Zalmay Khalilzad amesema Baraza la Usalama la UM yamkini likatoa taarifa juu ya mpango huo pengine hii leo .

“ Nadhani hili ni tokeo zuri”-alisema mjumbe huyo wa Marekani ,akaongeza, “Na sasa mpira uko katika lango la Sudan kuucheza.”

Sudan haikkukipinga kikosi hicho lakini wakuu wake mbali mbali walisema idadi ya kikosi hicho ni kubwa mno .Isitoshe, UM ugharimie na usimamie ki,kosi cha Umoja wan chi za kiafrika cha askari 7.000 katika mipango yake ,usafiri na kutoa huduma nyenginezo.

Mjumbe wa Sudan katika UM Abdelmahmood Abdelhaleem,aliiulamlamikia UM kwa kuituhumu Sudan kuchelewesha kuwekwa vikosi vya kuhifadhi amani huko Dafur wakati mipango ya UM wenyewe hata haikukamilika.

Hatahivyo, aliahidi kwamba serikali ya Khartoum itauchunguza mpango huo haraka iwezekanavyo.

Mpango huo mkubwa unadhihirisha shida ziliopo katika kuutimiza katika mkoa wenye ardhi ya ukame kama dafur ambako msaada wa serikali ya sudan katika kuwapatia askari hao maji na ardhi kwa kambi zao mara nyingi haupatikani hata kwa kikosi kidogo cha Um kiliopo huko tayari.

Jukumu mojawapo kuu ni kuwapatia usalama maalfu ya watu katika kambi na kusimamia njia za kuwafikishia shehena za misaada ya kibinadamu.Pia usalama kwa magari yanayolinda misafara ya shehena hiyo ambayo mara nyingi hushambuluiwa na kuporowa mali.

Kikosi hiki kipya lazima kiwe na uwezo wa kuzuwia fujo na matumizi ya nguvu.Mashauri juu ya mpango wa kuunda kikosi hiki, yana taratibu 2 za vikosi: Njia ya kwanza ni kuwa na jeshi la askari 19,500 kikijumuisha vikosi 18 na ya pili ni kuwa na jeshi la askari 17,605 likiwa na vikosi 15.

Kikosi cha polisi kitakuwa na jumla ya askari 3,772 na pengine kikosi kingine cha askari 2,500 kitakachokuwa na jukumu la kuanzisha na kukifunza kikosi maalumu cha polisi wa Dafaur kwenye kambi za wakimbizi.

Upungufu wa raslimali ulichochea balaa hili la Dafur miaka 4 iliopita pale waasi wasio wa asli ya kiarabu waliposhika silaha wakiituhumu serikali kutosikiza vilio vyao vya hali mbaya za kimaisha.

Serikali ya sudan hapo tena ikwapa silaha wasudan wa asili ya kiarabu na wa makabila mengine maarufu kwa jina la wanamgambo wa Janjaweed.Wakaanza ubakaji wa akina mama ,kuua na kupora mali.

Mwaka uliopita makabila ya kiarabu na yasio ya kirabu yakaanza kupigana wenyewe kwa wenyewe na kuvunja mapatano ya kusimamisha vita.Kiasi cha watu 200.000 wanakisiwa wameuwawa huko Dafur na zaidi ya milioni 2 wamepoteza maskani zao tangu mwaka 2003.

Kikosi hiki kipya, kimepangwa pia kulinda mipaka kati ya Sudan,Chad na Jamhuri ya Afrika ya kati ambako wakimbizi wameyakimbia maskani yao mpakani sana kutokana na kuandamwa na wanamgambo.Kwani, Sudan na Chad, kila moja inaungamkono waasi wa mwenziwe.