1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

KIGALI : Rwanda yakataa kushtakiwa kwa Kagame

21 Novemba 2006
https://p.dw.com/p/CCql

Rwanda leo hii imekataa wito uliotolewa na hakimu mmoja wa Ufaransa wa kumshtaki Rais Paul Kagame kutokana na madai ya kuhusika kwake na kifo cha aliekuwa kiongozi wa nchi hiyo Juvenal Habyarimana.

Waziri wa sheria Tharcisse Karugarama amesema madai hayo hayana msingi kabisa na kwamba hakimu huyo amechukuwa hatua hiyo kwa kuzingatia umbeya na uvumi.

Kifo cha Habyarimana kutokana na kuanguka kwa ndege hapo mwaka 1994 kilichochea mauaji ya kimbari ya Rwanda ambapo kwayo Watutsi 800,000 na Wahutu wa msimamo wa wastani waliuwawa katika kipindi cha miezi mitatu.

Hakimu huyo wa Ufaransa Jean-Louis Burguise hapo Ijumaa alipendekeza kwa mahkama ya Umoja wa Mataifa nchini Tanzania inayowashtaki watuhumiwa waliopanga mauaji hayo ya kimbari kwamba Kagame ambaye ni Mtutsi anapaswa kushtakiwa kutokana na kuhusika kwake kunakoshukiwa kwa kifo cha Habyarimana.

Waziri wa sheria wa Rwanda amemshutumu hakimu huyo wa Ufaransa kwa kucheza mchezo wa kisiasa juu ya madai hayo ambayo yatazidi kuharibu uhusiano ambao tayari ni mbaya kati ya serikali ya Rwanda na Ufaransa.