1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiev. Mawaziri wa ndani na mambo ya nje wafukuzwa kazi na bunge.

1 Desemba 2006
https://p.dw.com/p/CCnc

Bunge la Ukraine limepiga kura kuwafukuza mawaziri wa mambo ya ndani wa nchi hiyo pamoja na wa mambo ya kigeni, ambao ni washirika wa rais Viktor Yushchenko ambaye anaunga mkono mataifa ya magharibi.

Wabunge hao ambao wanatoka katika kambi yenye wabunge wengi wanaounga mkono Urusi, wameidhinisha azimio hilo kwa kura 247 wakimwondosha katika wadhifa wake waziri wa mambo ya kigeni Borys tarasyuk , mwasisi mkuu wa sera za rais wa Ukraine wa kuisogeza nchi hiyo karibu na mataifa ya magharibi na hata kuomba hatimaye kujiunga na umoja wa Ulaya na umoja wa NATO.

Hoja ya kumwondosha madarakani waziri wa mambo ya ndani Yuri Lutsenko, mtu mashuhuri katika mapinduzi ya mwaka 2004 yanayojulikana kama mapinduzi ya rangi ya chungwa, ambaye yalisaidia kumuingiza Yushchenko madarakani, ilipata kura 248.

Kura hizo mbili zimepindukia kiasi cha kura 226 zinazotakiwa kupitisha hoja katika bunge lenye wabunge 450. Rais Yushchenko ameshutumu hatua hiyo ya kuwaondoa washirika wake katika baraza la mawaziri kuwa ni kuiyumbisha Ukraine na kuapa kuwa atapambana na wale waliofanya kitendo hicho.