1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

KHARTOUM:Machafuko yanaendelea katika mji wa Khartoum kufuatia kifo cha John Garang.

2 Agosti 2005
https://p.dw.com/p/CEoU

Hali imezidi kuwa ya wasiwasi nchini Sudan baada ya kuripotiwa kuongezeka kwa machafuko kufuatia kifo cha Makamu wa Rais wa nchi hiyo John Garang,aliyekufa baada ya helikopta yake kuanguka siku ya Jumapili nchini Uganda.

Katika kitongoji kimoja cha mji wa Khartoum watu kadhaa wameuawa kufuatia mapigano baina ya watu wa maeneo ya kusini na kaskazini mwa Sudan.

Hadi sasa watu 34 wameripotiwa kuuawa katika ghasia zilizotokea baada ya kutangazwa rasmi kifo cha Bwana Garang.

Wakati huo huo Makamu wa Bwana Garang Salva Kiir,ameteuliwa na chama chake cha Sudan People’s Liberation Movement-SPLM kuchukua nafasi iliyoachwa na Bwana Garang.Chama hicho kina kila matumaini kuwa Bwana Kiir ataapishwa kuwa Makamu wa Rais wa Sudan katika kipindi cha wiki mbili zijazo.

Viongozi mbalimbali duniani wamekuwa wakipongeza jitahada zilizofanywa na Bwana Garang za mchakato wa kuleta amani ya Sudan.

Nae Rais George Bush wa Marekani amewatolea wito raia wa Sudan kujiepusha na vitendo vya vurugu kwa wakati huu.