1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Khan autaka ulimwengu kuchukua hatua kuhusu Kashmir

Yusra Buwayhid
6 Agosti 2019

Waziri Mkuu wa Pakistan Imran Khan anafikiria kulalamika katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, baada ya India kubatilisha kifungu cha katiba kinacholipa mamlaka maalumu eneo la Kashmir linalosimamiwa na India.

https://p.dw.com/p/3NSB4
Kyrgyzstan Gipfeltreffen Imran Khan
Picha: picture-alliance/AP Photo/Sputnik/A. Druzhinin

Akiwa katika kikao cha dharura kilichoitishwa bungeni katika mji mkuu wa Islamabad, Khan amesema leo kuwa wanataka viongozi wa dunia kuzingatia kinachoendelea.

"Tutapambana katika kila jukwaa. Tunafikiria namna ya kulifikisha hili katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa," amesema Khan.

Khan pia amewahimiza viongozi wa kimataifa kuingilia kati uamuzi huo wa India, ambao umeongeza wasiwasi wa kuzuka machafuko kati ya majirani hao mawili wenye kumiliki silaha za nyuklia na ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakizozania eneo hilo la Kashmir.

Hapo jana serikali ya India ilitangaza kuwa itabatilisha kipengele cha katiba ambacho kinalipa kiasi fulani cha uhuru eneo la Kashmir linalosimamiwa na India katika milima ya Himalaya.

Soma zaidi: Bunge la India kuidhinisha sheria mpya kuhusu Kashmir

Pakistan imepinga hatua hiyo na kusema kuwa inakiuka maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, huku ikitishia kufanya kila linalowezekana kuilazimisha India kubadilisha uamuzi wake huo.

Khan pia ameeleza kwamba kubadilisha sheria zilizopo kutaongeza mvutano kati ya India na Pakistan na kusababisha mgogoro mkubwa zaidi.

Indien Kaschmir-Konflikt nach Änderung Artikel 370
Wanajeshi wapiga doria mitaa ya Jammu eneo la Kashmir, kufuatia uamuzi wa IndiaPicha: AFP/R. Bakshi

Baada ya mkutano na makamanda wa juu katika jiji la Rawalpindi, Mkuu wa Jeshi la Pakistan, Jenerali  Qamar Javed Bajwa amesema leo kwamba watawaunga mkono watu wa Kashmir, na wamejiandaa kutekeleza wajibu wao katika suala hilo kwa hali yoyote.

Wanasiasa wa Kashmir wafichwa maandalizi ya uamuzi wa India

Kila upande unadai mamlaka kamili ya eneo la Kashmir lenye waumini wengi wa Kiislam lakini kwa sasa kila nchi inasimamia sehemu tu ya eneo hilo. Eneo la Kashmir limegawanywa, sehemu moja inayojulikana kama  Jammu na Kashmir inasimamiwa na India na sehemu nyingine ya Azad Jammu na Kashmir inasimamiwa na Pakistan.

Wanasiasa wa eneo hilo la Kashmir linalosimamiwa na India wamesema walifichwa kuhusu uamuzi huo. Viongozi watatu waliozungumza na shirika la habari la Reuters wakiwa majumbani mwao katika mji mkuu wa Srinagar wa  Jammu na Kashmir wamesema walikuwa hawana taarifa zozote juu ya kinachoendelea.

Majirani hao wawili wenye kumiliki silaha za nyuklia wameshawahi kupigana mara tatu tofauti juu ya eneo hilo la Kashmir. Na mnamo mwezi Febuari walipambana kwa mapigano ya angani kufuatia kundi la wanamgambo lenye makao yako Pakistan kudai kuhusika na shambulizi dhidi ya ujumbe wa kijeshi wa India.

Chanzo: rtre,pda