1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kesi ya Tundu Lissu dhidi ya spika Ndugai yaanza kusikilizwa

Hawa Bihoga 15 Agosti 2019

Aliyekuwa mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, ameiomba Mahakama Kuu kutoa amri ya kusitisha zoezi la kuapishwa kwa mbunge mteule wa jimbo hilo, Miraji Mtaturu, ambaye alichaguliwa takriban mwezi mmoja uliopita.

https://p.dw.com/p/3Nx1P
Tansania Dar es Salaam Oberstes Gericht verhandelt über Ex-Angeordneten Tundu Lissu
Picha: DW/Said Khamis

Mahakama kuu nchini Tanzania imeanza kusikiliza shauri la Tundu Lissu dhidi ya spika wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, baada ya kumvua ubunge wake kwa madai kuwa amekiuka masharti ikiwemo kutohudhuria bungeni kwa kipindi kirefu bila spika kuwa na taarifa naye. 

Jopo la wanasheria wanne wanaomtetea Lissu limewasilisha maombi matano ya mlalamikaji , wakiongozwa na Wakili Peter Kibatala katika shauri la madai nambari 18 la mwaka 2019, dhidi ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Ndugai na mwanasheria mkuu wa serikali,  ili apate amri ya mahakama kuhusiana na kuvuliwa ubunge wake aliotumikia kwa takriban mwaka mmoja na nusu kabla ya kupigwa risasi katika mji mkuu wa Tanzania, Dodoma.

Tansania Dar es Salaam Oberstes Gericht verhandelt über Ex-Angeordneten Tundu Lissu
Wakili Peter Kibatala anayemtetea Tundu Lissu katika kesi ya kuvuliwa ubungePicha: DW/Said Khamis

Yapi ni madai ya Lissu?

Lissu anaitaka Mahakama Kuu kutoa amri kadhaa ikiwemo ya kumuamuru Spika wa Bunge Job Ndugai kuwasilisha mahakamani taarifa ya uamuzi wa kumvua ubunge aliyoitoa bungeni, ili iweze kuupitia na kisha iamuru kuutengua na kuutupilia mbali.

Miongoni mwa maombi mengine ni mahakama imwamuru Spika ampatie Lissu nakala ya taarifa ya kumvua ubunge pamoja na amri ya kusitishwa kuapishwa kwa mbunge mteule wa jimbo hilo, Miraji Mtaturu, wa Chama cha Mapinduzi CCM, ambaye alitangazwa kuwa mbunge bila kupingwa mwezi uliopita. 

Mawakili wa serikali

Tundu Lissu azungumzia maamuzi ya kuvuliwa ubunge

Lakini ombi hilo limepingwa vikali na jopo la mawakili wa Serikali wakiongozwa na Wakili Vicent Tango, wakidai kuwa kwa sasa sio muda muafaka wa kuanza kulisikiliza. Aidha wameiomba mahakama muda wa siku nane ili waweze kuwasilisha hati ya kiapo kinzani, pamoja na hati ya maelezo kinzani kabla ya maombi hayo kupangiwa siku ya kuanza kusikilizwa rasmi, kwa kuwa shauri hilo linahusisha mhimili mwingine, ambayo ni Bunge, hivyo wanahitaji muda wa kushauriana na Spika ili kuweza kuandaa kiapo kinzani.

Hakimu anayesikiliza shauri hilo, Sirilius Matupa, alihairisha shauri hilo kwa takriban dakika arobaini na tano na kisha kurejea na maamuzi ya kuhairisha shauri hilo hadi tarehe 23 Agosti ambapo atasikiliza maombi ya Lissu, likiwemo la kusitisha zoezi la kuapishwa kwa mbunge mteule na kisha kutoa maamuzi.

Tansania Parlament in Dar es Salaam | Job Ndugai, Sprecher
Spika wa bunge la Tanzania Job NdugaiPicha: DW/E. Boniphace

Nje ya Mahakama 

Katibu mkuu wa chama kikuu cha upinzani CHADEMA, ambacho anatoka Tundu Lissu, Vicent Mashinji, aliwaambia waandishi wa habari kuwa wao kama chama ndio wadhamini wa ubunge wa Lissu hivyo wanaunga mkono hatua ya Lissu kuitafuta haki.

"Kama mnavyojua katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inasema huwezi ukagombea cheo chochote cha kiserikali kama hujadhaminiwa na chama cha siasa. Kwahiyo Lissu anatokana na chama cha Demokrasia na Maendeleo, kwahiyo maanuzi yaliyofanyika ya kumvua ubunge yanaathiri moja kwa moja CHADEMA, hivyo sisi tunasimama naye na leo ndio shauri lake kwanza limeanza", alisema Mashinji katibu mkuu wa CHADEMA. 

Kupitia kwa mawakili wake, Lissu anaiomba mahakama hiyo isikilize na kutoa uamuzi wa maombi yake haraka kwani vinginevyo Mtaturu ataapishwa kushika wadhifa huo kabla ya haki kutendeka.

Hawa Bihoga, Dar es salaam