1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kerry kuhimiza kupambana na Mabadiliko ya Tabianchi China

17 Julai 2023

Mjumbe Maalum wa Marekani wa Mabadiliko ya Tabianchi, John Kerry, yuko nchini China akinuwia kufufua mazungumzo yaliyokwama baina ya madola hayo mawili juu ya kupunguza viwango vya utoaji wa gesi chafuzi kwa mazingira.

https://p.dw.com/p/4TzXh
China | John Kerry akikutana na Xie Zhenhua
Mjumbe Malaamu wa Marekani kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi, John Kerry (kushoto) akisalimiana na mwenzake wa China, Xie Zhenhua kabla ya kuanza kwa mazungumzo yao mjini Beijing.Picha: Valerie Volcovici/REUTERS

Vyombo vya habari vya China vimeripoti kuwa hadi mchana huu, Kerry alikuwa tayari amekutana na mwenzake wa China anayeshuhgulikia masuala ya mabadiliko ya tabianchi, Xie Zhenhua mjini Beijing.

Walizungumza kwa muda wa saa nne lakini taarifa zaidi ya kile kilichojadiliwa bado hakijawekwa wazi. 

Serikali mjini Beijing imesema mabadiliko ya tabianchi ni changamoto ya pamoja na inafaa kukabiliwa na kila mmoja duniani na ndiyo maana China iko tayari kubadilishana mawazo na Marekani na kufanya kazi kushughulikia janga hilo.

Mtazamo huo wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya China unaonesha jinsi mabadiliko ya tabianchi lilivyo jambo la dharura kiasi hata mataifa hayo mawili ambayo yanazingatiwa kuwa mahasimu yanaona ni busara kushirikiana.

Ziara inafuatia diplomasia iliyoingia doa mwaka 2022

China | John Kerry akutana na Xie Zhenhua
Mjumbe Malaamu wa Marekani kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi, John Kerry akihudhuria mazungumzo na mwenzake wa China, Xie Zhenhua mjini Beijing.Picha: Valerie Volcovici/REUTERS

Kerry, ambaye ni waziri wa zamani wa mambo ya kigeni wa Marekani, amemudu kuivutia China na amefanikiwa kuendeleza ushirikiano na nchi hiyo hata katika wakati mahusiano kati ya Washington na Beijing yalitetereka.

Hata hivyo mazungumzo baina ya nchi hizo mbili yaliingia doa na kusitishwa kwa muda mwaka jana baada ya Spika wa zamani wa Baraza la Wawakilishi la Bunge la Marekani, Nancy Pelosi kufanya ziara kwenye kisiwa cha Taiwan, safari iliyoikasirisha sana China.

Safari ya Kerry mara hii inalenga kuyafufua mazungumzo hayo ya kidiplomasia baina ya nchi hizo mbili ambazo ndiyo watoaji wakubwa wa gesi chafuzi kwa mazingira zinazochangia mabadiliko ya tabianchi.

China yenyewe imeweka lengo la kupungaza kwa kiwango cha chini kabisa utoaji wa gesi ya ukaa au kaboni ifikapo mwaka 2030, na ifikapo 2060 nchi hiyo inadhamiria kutotoa hata chembe ya gesi chafuzi.

Lakini uamuzi wa hivi karibuni wa China wa kuongeza kiwango cha matumizi ya makaa ya mawe ulizusha mashaka kuwa mipango yake ya kupunguza uchafuzi haitatimia.

Akiwa mjini Beijing, Kerry anatarajiwa kuihimiza China kupunguza utegemezi wake kwenye nishati ya makaa ya mawe na kuweka malengo ya kupunguza utoaji wa gesi nyingine hatari iitwayo Metani ambayo pamoja na gesi ya Kaboni ndizo zinachangia pakubwa ongezeko la joto kwenye uso wa dunia.

Je, Kerry atafanikiwa kurekebisha mahusiano kati ya nchi mbili kuhusu mazingira?

Symbolbild Heißester Juni seit Wetteraufzeichnung
Mabadiliko ya Tabianchi yanaongezeka kiwango cha joto kwenye uso wa duniaPicha: Manu Fernandez/AP/picture alliance

Safari ya mwanadiplomasia huyo nchini China inafanyika wakati kuna hamkani miongoni mwa wanasiasa nchini Marekani ambao wanadhani Beijing haifanyi vya kutosha kutimiza wajibu wake wa kupunguza utoaji wa gesi chafuzi.

Tiketi yake ya kwenda Beijing haikupatikana bila vizingiti. Alhamisi iliyopita Kerry aliitwa mbele ya Kamati ya Mambo ya Kigeni ya Bunge la Marekani kufafanua ni vipi diplomasia inaweza kuishawishi China kuchukua jukumu kubwa zaidi kuhusu mabadiliko ya tabianchi.

Ziara yake nchini China ni mwendelezo wa juhudi za pande hizo mbili kurekebisha mahusiano yao yaliyopwaya.

Inafuatia nyingine zilizofanywa na maafisa wa ngazi ya juu wa Marekani mjini Beijing ikiwemo waziri wa mambo ya kigeni Antony Blinken.

Lakini haifahamiki iwapo mahusiano hayo yanayoengwa engwa yatadumu kwa muda mrefu. Kwa sababu masuala tete yanayochochea mivutano baina yao bado yapo.

Mathalani hii leo Taiwan imesema mnamo mwezi unaokuja, makamu wake wa rais atapitia nchini Marekani akiwa njiani kwenda Paraguay kuhudhuria dhifa ya taifa ya kuapishwa rais mpya.

Uamuzi wa aina hiyo wa kusimama nchini Marekani kwa maafisa wa Taiwan mara zote umesababisha malalamiko kutoka China, inayokizingatia kisiwa hicho kuwa sehemu ya himaya yake na haitaki kiwe na mahusiano ya kidiplomasia na nchi yoyote duniani.

Lakini kwa Washington inaonesha imetia pamba masikio hasa linapokuja suala la hadhi ya Taiwan.