1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenyatta na Samia washuhudia utiaji saini mikataba mipya

George Njogopa10 Desemba 2021

Marais Samia Suluhu wa Tanzania na Uhuru Kenyatta wa Kenya wamesisitiza haja ya nchi zao kuendelea kuondoa vikwazo vinavyodumaza mahusiano mema kwa pande zote mbili.

https://p.dw.com/p/446gI
Kenia Nairobi | Besuch Samia Suluhu Hassan, Präsidentin Tansania | mit Uhuru Kenyatta
Picha: Simon Maina/AFP/Getty Images

Viongozi hao wamesisitiza hayo ikulu jijini Dar es salaam, wakati Rais Uhuru akiwa katika ziara ya kiserikali na ya mwisho nchini humu kama kiongozi kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu nchini mwake hapo mwakani.

Rais Samia aliyekuwa wa kwanza kuzungumza mbele ya waandishi wa habari ameitaja Kenya kama ndugu, rafiki na jamaa ambaye hapaswi kununiwa hata kunapojitokeza hali yoyote ya sintofahamu.

Kama sehemu ya kuimarisha mahusiano na ujirani mwema, nchi hizo zimewekeana saini mikataba inayotoa manufaa kwa pande zote na baadhi ya mikataba hiyo ni ile inayolenga sekta za kibiashara, afya, uwekezaji na ubadilishanaji wafungwa.

Rais Samia amesema makubaliano hayo yanalengo la kuzifanya pande zote mbili zinakaribiana zaidi kiuchumi na biashara.

Miradi ya pamoja

Mpaka wa Namanga baina ya Tanzania na Kenya
Mpaka wa Namanga baina ya Tanzania na KenyaPicha: Veronica Natalis/DW

Viongozi hao ambao hivi karibuni walikutana kwa mara ya kwanza ikulu ya Nairobi walikozungumzia masuala mbalimbali, walijadiliana pia namna wanavyoweza kudumisha uhusiano mwema na baadae walipeana zawadi

Ujenzi wa miundombinu ya barabara, bomba la usafirishaji gesi itakayotoka Tanzania hadi Mombasa ni maeneo mengine ambayo yameafikiwa.

Rais Uhuru Kenyatta aliyekuwa nchini tangu jana kuhudhuria kilele cha maadhimisho ya miaka 60 ya uhuru wa iliyokuwa Tanganyika, anasema kuondoa vikwazo ni jambo  maana kwa uchumi wa pande zote.

Kuhusu vikwazo vilivyosalia, marais hao wamewaagiza mawaziri wao kuendelea kujadiliana ili kuhakikisha vyote vinaondolewa. Hadi mapema mwaka huu, jumla ya vikwazo 64 vya kibiashara vilikuwa vikiendelea kutatiza pande zote mbili lakini baada ya majadiliano ya hivi karibuni, tayari vikwazo 46 vimeondolewa.