1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya yazuia filamu nyingine ya mapenzi ya jinsia moja

Thelma Mwadzaya24 Septemba 2021

Kwa mara ya pili serikali ya Kenya imepiga marufuku filamu inayoangazia masuala ya mapenzi ya jinsia moja iitwayo “I am Samuel”. Bodi ya filamu KFCB ilitangaza kuwa filamu hiyo haifai kutazamwa na wakenya kwani inakiuka maadili na katiba. Filamu hiyo ilionyeshwa kwa mara ya kwanza mwezi wa Oktoba mwaka jana kwenye tamasha la 64 la filamu la London, BFI.

https://p.dw.com/p/40oxe

Kwenye taarifa yake, bodi ya filamu nchini Kenya, KFCB, ilibainisha kuwa filamu ya “I am Samuel” haifai kuonyeshwa kwa umma kwani inasukuma hoja ya kuwa na ndoa za jinsia moja na kuzikubali kinyume na ibara ya 165 ya sheria ya filamu na uigizaji.

Sheria hiyo inapiga marufuku mapenzi ya jinsia moja. Abbas Suleiman amefanya kazi na vijana walio kwenye uhusiano wa mapenzi ya jinsia moja na huu ndio ushauri wake kwa serikali

Kulingana na bodi ya filamu ya Kenya, KFCB, wasanii wa filamu ya “I am Samuel” wanaashiria kuwa wanafunga ndoa halali ya kidini jambo ambalo ni kufuru. Itakumbukwa kuwa Oktoba iliyopita, akihojiwa na shirika la habari la AFP ,Samuel Murimi aliyeiandaa na kuiongoza filamu hiyo alielezea kuwa sanaa iliyotulia na kwamba inaashiria hali halisi ya familia iliyo na mtoto wa kiume anayekumbatia mapenzi ya jinsia moja. Sam Githaiga ana mpenzi wake wa kiume na familia yake haijamkubali.

Alilazimika kukimbia nyumbani na huu ndio mtazamo wake wa filamu za kuangazia masuala ya mapenzi ya jinsia moja zinapopigwa marufuku.

Ifahamike kuwa mapenzi ya jinsia moja ni marufuku katika mataifa mengi barani Afrika. Adhabu ya kuwa katika uhusiano wa mapenzi ya jinsia moja ni kifungo cha miaka 14 jela. 

Katika nchi nyingi za Afrika, adhabu ya kuwa katika uhusiano wa mapenzi ya jinsia moja ni kifungo cha miaka 14 jela. 
Katika nchi nyingi za Afrika, adhabu ya kuwa katika uhusiano wa mapenzi ya jinsia moja ni kifungo cha miaka 14 jela. Picha: Lev Dolgachov/Zoonar/dpa/picture-alliance

Hii si mara ya kwanza kwa filamu inayoangazia masuala ya mapenzi ya jinsia moja kupigwa marufuku nchini Kenya.

Mwaka 2018, filamu ya Rafiki ilikuwa ya kwanza kuonyeshwa kwenye tamasha la Cannes la Ufaransa kabla ya kupigwa marufuku kwa watazamaji wa Kenya.

Filamu ya Rafiki iliangazia mapezi ya jinsia moja kati ya wanawake. Filamu ya “I am Samuel” iliyo na urefu wa dakika 52 imeandaliwa na kuelekezwa na Samuel Murimi aliye na uzoefu wa kuandaa vipindi na tamthilia.