1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya yatangaza tahadhari ya Ebola Busia

22 Septemba 2022

Wizara ya afya nchini Kenya imeweka tahadhari kwenye mpaka wake na Uganda baada ya taifa hilo kuripoti maambukizi ya ugonjwa wa Ebola, Shirika la Afya duniani WHO likitangaza mripuko wa Ebola nchini Uganda

https://p.dw.com/p/4HD8w
Uganda Mpondwe | Medizinisches Personal misst Temperatur - Ebola-Epidemie im Kongo
Picha: picture-alliance/dpa/AP/R. Kabuubi

Kwenye tahadhari hii, Kenya imeagiza vipimo miongoni makundi mbali mbali ya watu huku wakaazi wa eneo la Busia linalopakana na Uganda wakiwa na wasiwasi juu ya kusambaa maambukizi kwenye eneo hilo.

Wasiwasi huo umefuatia ripoti za kuzuka maambukizi  ya virusi vya ugonjwa wa Ebola katika wilaya ya Mubenda katika nchi jirani ya Uganda.

Raia hawa, wamehusisha wasi wasi wao kutokana na kile wanachodai ni mpaka unaotumiwa na watu wanaoingia na kutoka kwa  njia za mikato  kati ya mataifa haya mawili na hivyo kuhimiza serikali kupitia wizara ya afya kuimarisha zaidi juhudi za kufanya vipimo miongoni mwa wasafiri hasahasa wanaoingia Kenya kutoka Uganda.

Wahudumu wa boaboda, madereva wa lori za kusafirisha mizigo nje ya nchi wametajwa kuwa katika nafasi hatari ya kusambaza virusi hivyo endapo mikakati inayowekwa ya kuzuia haitazingatiwa.

Wahudumu wa bodaboda wanakuwa na uwepesi wa kukiri usafirishaji wa abiria kati ya mataifa haya.

Waziri wa afya nchini Kenya Mutahi Kagwe amezitaka serikali za majimbo yaliyokaribu na Uganda kuimarisha mikakati ya dharura kusaidia kutambua dalili za Ebola.

Mikakati mingine iliyowekwa ni pamoja na Uhamasishaji wa jamii za mpakani, vipimo miongoni mwa watu walio kwenye hatari zaidi ya maambukizi; madereva, wahudumu wa afya miongoni mwa mikakati mingine ya kuzuia ugonjwa huo ambao dalili zake ni joto mwilini, kuendesha, kutapika, macho mekundu, maumivu ya kichwa na ndani ya shingo, kutokwa na damu miongoni mwa dalili nyingine.

Musa Naviye, DW Kisumu