1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UchumiChina

Kenya yasaka mikopo zaidi kutoka China

16 Oktoba 2023

Viongozi wa mataifa yanayoinukia kiuchumi wanakutana nchini China kwa kongamano ambalo litaadhimisha miaka 10 ya mradi wa kimataifa wa ujenzi wa miundombinu ya reli na barabara, huku Kenya ikisaka mikopo zaidi.

https://p.dw.com/p/4XbCL
Rais wa Kenya- William Ruto akizungumza wakati wa kongamano la kwanza la Afrika la  hali ya hewa jijini Nairobi mnamo Septemba 4, 2023
Rais wa Kenya- William RutoPicha: Khalil Senosi/AP/picture alliance

Zaidi ya viongozi kumi na mbili kutoka Afrika, Asia na Mashariki ya Kati wamewasili mjini Beijing kwa kongamano hilo la  Belt and Road Initiative (BRI) wakitanguliwa na Rais Gabriel Boric wa Chile na Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orbán siku ya Jumapili (Oktoa 15).

Soma pia: Marekani imekua ikichukua njia mbalimbali za kukabiliana na ushawishi wa China unaozidi kuongezeka

Viongozi waliowasili siku ya Jumatatu (Oktoba 16) ni pamoja na Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed, Rais Ranil Wickremesinghe wa Sri Lanka na  mwenzake wa Jamhuri ya Kongo, Denis Sassou Nguesso, Waziri Mkuu wa Papua New Guinea James Marape na mwenzake wa Cambodia, Hun Manet.

Rais Vladimir Putin wa Urusi na wawakilishi wa serikali ya Taliban nchini Afghanistan pia wanatarajiwa kuhudhuria kongamano hilo.

Rais wa Kenya atafuta mkopo zaidi kutoka China

Katika hatua nyingine, Rais William Ruto wa Kenya ambaye pia anahudhuria kongamano hilo anatafuta mkopo wa dola bilioni moja kutoka China, licha ya kuongezeka kwa deni la umma la nchi hiyo ambalo sasa limefikia dola bilioni 70. Hii ni kulingana na takwimu za hazina ya kitaifa ya mwaka 2022/2023.

Rais wa China Xi Jinping akitoa hotuba wakati wa hafla ya ufunguzi wa kongamao la BRI mjini Beijing mamo Aprili 26, 2019
Rais wa China Xi JinpingPicha: Kyodo/picture alliance

Taarifa kutoka kwa Msemaji wa Ikulu ya Kenya, Hussein Mohammed, ilisema kuwa rais huyo angelitoa hotuba muhimu chini ya mada ‘Uchumi wa kidigitali kama chanzo kipya cha ukuaji'  wakati wa mkutao huo wa kilele.

Taarifa hiyo imeendelea kusema kuwa Rais Ruto pia angelishiriki katika mkutano wa wafadhili wa Kenya ili kusisitiza nafasi ya Kenya kama eneo la uwekezaji kwa kampuni za China .

Moja ya miradi chini ya BRI ni ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR

Moja ya miradi maalumu chini ya mpango huo wa BRI nchini Kenya, ni ujenzi wa reli ya kisasa wa SGR inayoanzia kutoka mji wa bandari wa Mombasa hadi Bonde la Ufa kupitia mji mkuu, Nairobi.

Ujenzi wa mradi huo uligharimu dola bilioni 4.7 lakini umekabiliwa na changamoto nyingi, zikiwemo ucheleweshaji na kiwango cha chini cha huduma ya usafirishaji mizigo.

Kulingana na takwimu za kitaifa, Kenya imekuwa ikipambana na deni la umma linaloongezeka huku dola bilioni 6 zikiwa deni la China. Muda wa kulipa baadhi ya madeni ya nchi hiyo ni kipindi cha fedha cha 2023/2024 hali inayozidisha shinikizo zaidi kwa serikali.

Hata hivyo, haijakuwa wazi ikiwa rais  Ruto na ujumbe wake wataruhusiwa kuwa na mpangilio mpya wa kulipa madeni hayo ama kuongezewa muda wa malipo ya riba.