1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya yaiaga rasmi noti ya zamani ya shilingi 1,000

Thelma Mwadzaya1 Oktoba 2019

Wakenya wameiaga rasmi noti ya zamani ya shilingi alfu moja iliyopoteza thamani baada ya muda wa kuzisalimisha benki kufikia kikomo. Hata hivyo idadi kamili ya noti zilizokusanywa na serikali bado haijajulikana

https://p.dw.com/p/3QXyv
Kenia Währung Schilling Geldscheine
Picha: Getty Images/AFP/S. Maina

Hata hivyo idadi kamili ya noti zilizokusanywa na serikali haijajulikana bado. Operesheni hiyo ilianza miezi mine iliyopita ili kupambana na uhalifu na vitendo vya kughushi pesa.

Noti hiyo ya zamani ya shilingi alfu moja ilipoteza thamani yake usiku wa kuamkia leo 01.10.2019  na benki zote zilitakiwa kuwasilisha idadi zilizonazo kwa benki kuu ya Kenya. Kwa sasa hakuna atakayeweza kuokoa noti hizo iwapo anazo na Benki kuu ya Kenya inasubiri kuziharibu zisiweze kurejeshwa kwenye mfumo wa mzunguko wa pesa nchini humo.

Gavana wa benki kuu ya Kenya Dr Patrick Njoroge alisisitiza kuwa muda wa kukusanya noti za zamani za alfu moja hautaongezwa. Baadhi ya viongozi wamelipinga hilo na kuitaka serikali kubadili msimamo wake.

Wanaohifadhi pesa kwa njia zisizoeleweka kuchunguzwa

Kulingana na Benki kuu ya Kenya, benki zimekuwa chonjo kuwakagua wanaohifadhi pesa kwa njia zisizoeleweka na kuwasilisha majina yao kwa vyombo vya serikali vya uchunguzi. Kiasi cha akaunti 900 za benki zimemulikwa hadi sasa. Takwimu za Benki Kuu zilibaini kuwa noti milioni 216 za alfu ya zamani zilikuwa mikononi mwake mwezi wa Juni.

Kadhalika idadi ya noti nyingine za zamani ambazo bado zinatumika imeongezeka. Noti hizo ni za shilingi 50, 100,200 na 500.

Kufikia jana ambapo muda wa mwisho ndio ulifikia kikomo, waliopeleka benki zaidi ya shilingi milioni 2 hawakuzidi 24. Ifahamike kuwa mwezi mmoja tu baada ya tangazo la kusitisha matumizi ya noti ya zamani ya alfu kutolewa, shilingi bilioni 25 zilirejeshwa kwenye mfumo wa pesa na benki katika jitihada za kutimiza agizo.

Hapo kesho, Gavana wa benki kuu ya Kenya anatazamiwa kuweka bayana idadi kamili ya noti ilizokusanya na iwapo wahalifu wowote wamenaswa katika kipindi cha miezi minne ya kusomba pesa hizo.