1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya yadhamiria kudhibiti vurugu za uchaguzi

Admin.WagnerD4 Agosti 2022

Serikali ya Kenya inaazimia kuziba mianya yote ya ukosefu wa usalama kipindi hiki cha uchaguzi, huku hatua ya hivi punde ikiwa kuzinduliwa kwa kituo kikuu cha usalama jijini Nakuru.

https://p.dw.com/p/4F75T
Kenia Wahlen 2022
Picha: Yasuyoshi Chiba/AFP

Kituo hicho kinaunganisha mawasiliano ya maafisa wa usalama na wananchi wa kaunti kumi na nne za bonde la ufa. Kwenye mchakato wa kubaini maeneo yaliyo na uwezekano wa machafuko ya kisiasa kipindi hiki cha uchaguzi mkuu, mengi ya maeneo yaliyotajwa na Tume ya kitaifa ya uwiano na utangamano, NCIC, yanapatikana eneo la Bonde la Ufa yakiwemo Naivasha, Nakuru na Eldoret.

Wizara ya usalama wa ndani imezindua kituo cha usalama jijini Nakuru kitakachowawezesha kuyakabili kwa haraka matukio yanayotishia usalama. Maalim Mohammed, kamishna wa kanda ya Bonde la Ufa amewarai wananchi kutosita kutoa ripoti kwa walinda usalama.

Kuna ishara ya kufanyika vurugu tarehe sita mwezi huu.

Kenia Wahlen 2022
Makasha ya karatasi za kupiga kuraPicha: Yasuyoshi Chiba/AFP

Katika taarifa yake amesema ''Tumebaini pia kwamba, na unajua serikali ina njia za kupata taarifa, tunajua kuna makundi kwenye jamii yanayopanga kufanya mikutano baada ya tarehe sita mwezi huu. Ni bayana kulingana na sheria kwamba mikutano ya mwisho ya kisiasa inapaswa kufanyika kabla ya saa kumi na mbili jioni, tarehe sita mwezi huu. Kama una ujumbe wowote kwa Wakenya, hakikisha umeutoa kabla ya muda huo wa mwisho uliowekwa.''

Siku mbili zilizopita waziri wa usalama wa ndani Fred Matiangi, alizuru eneo la Nakuru ambapo alikutana na asasi za usalama kutoka kaunti kumi na nne za Bonde la Ufa kwa minajili ya kupanga mikakati ya usalama wakati huu wa uchaguzi. Matiangi alieleza kwamba maafisa zaidi wa usalama wamepelekwa kwenye mji wa Eldoret, na maeneo ya Kuresoi na Nessuit kaunti ya Nakuru kuimarisha usalama.

Eneo la Bonde la Ufa ni ngome yake Naibu Rais William Ruto.

Ruto na wafuasi wake wa mrengo wa Kenya Kwanza wameishutumu serikali kwa njama ya kuibua hofu kati ya wafuasi wake eneo la Bonde la Ufa ili kuwatisha watu kujitokeza kupiga kura siku ya uchaguzi. Hata hivyo, Kamishna Maalim amewahakikishia wakaazi wa eneo la Bonde la Ufa usalama kipindi hiki cha uchaguzi.

Zaidi anasema ''Eneo la Bonde la Ufa halitawahi kushuhudia yale yamekuwa yakitokia wakati wa chaguzi zingine, hiyo itakuwa historia. Tumejitolea kuhakikisha uchaguzi huu unakuwa huru bila vitisho au udhalimu kutoka kwenye chama chochote cha kisiasa.''

Soma zaidi:Uchaguzi wa Kenya watumbua upya makovu ya ufisadi

Tume ya NCIC inaendesha kampeni ya amani kwenye mitandao ya kijamii kupitia hashtag #Elections bila noma, ili kuwashawishi hasa vijana kukumbatia amani kipindi hiki. Wakio Mbogho DW, Nakuru.

 

DW-Nakuru