1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya yaanza uhamasishaji kuhusu haki za kiuchumi na kijamii

Wakio Mbogho22 Oktoba 2018

tume ya haki za kibinadamu nchini Kenya inatoa maelekezo jinsi serikali za kaunti zinavyoweza kuwajibika kuhakikisha haki za watu wake zimezingatiwa.

https://p.dw.com/p/36x9V
Kenia KNCHR Benard Mogesa
Picha: DW/W. Mbogo

Tume ya haki za kibinadamu nchini Kenya imeanza mchakato wa kuzihamasisha serikali za kaunti kuhusu utekelezaji wa haki za kiuchumi na kijamii. Kupitia mswada uliowasilishwa kwenye seneti, tume hiyo inalenga kuzijumuisha serikali za kaunti kuhakikisha kila mkenya anapata huduma za msingi kama vile afya, elimu na lishe bora ili kuona hadhi ya kibinadamu imeimarishwa.

Haki ya kiuchumi na kijamii ni swala ambalo halijapewa uzito na uongozi licha ya umuhimu wake katika maisha ya kila siku ya mwananchi. Maeneo ya kaskazini mashariki na baadhi ya sehemu za bonde la ufa yameathirika pakubwa - wengi wa wakaazi wake wakikosa uwezo wa kupata huduma msingi kama vile chakula, elimu na afya.

Ni kwa sababu hii, tume ya kitaifa ya haki za kibanadamu nchini Kenya imeanza mchakato wa kuzihamasisha serikali za kaunti kuhusu utekelezaji wa haki za kiuchumi na kijamii kwa minajili ya kulinda hadhi ya kibinadamu.

Katika kikao kilichowaleta pamoja maafisa wa kaunti 15 nchini Kenya, tume hiyo inatoa maelekezo jinsi serikali za kaunti zinavyoweza kuwajibika kuhakikisha haki za watu wake zimezingatiwa. Mswada huo waliouwasilisha katika bunge la seneti, unaotoa mwongozo wa utekelezaji wa sheria hiyo kama ilivyoainishwa katika kipengee cha 43 cha katiba ya Kenya.

Aliyekuwa seneta wa Mombasa na pia kamishna wa zamani wa tume ya kitaifa ya haki za binadamu KNCHR Hassan Omar
Aliyekuwa seneta wa Mombasa na pia kamishna wa zamani wa tume ya kitaifa ya haki za binadamu KNCHR Hassan OmarPicha: DW/W. Mbogo

Haki ya kupata kiwango cha juu cha kuimarika kiuchumi na kijamii

Kwa mujibu wa sheria hiyo, kila Mkenya ana haki ya kupata kiwango cha juu cha kuimarika kiuchumi na kijamii kwa kuhakikisha hakosi chakula, huduma za afya, makaazi bora, mazingara safi, elimu na usalama.

Aliyekuwa seneta wa Mombasa Hassan Omar na ambaye pia ni mmoja wa maafisa waliotunga mswada huo, anaonya serikali dhidi ya kutegemea takwimu kuelezea hali ya kiuchumi ya wananchi. Kulingana naye changamoto za kila kaunti hazifanani kwa hivyo kaunti zinazopaswa kuyapa kipau mbele matatizo ya maeneo yao, kulingana na uzito kwa watu wake. Omar ameendelea kusema

"Jambo ambalo ni la kupewa kipau mbele mandera huenda si la kupewa kipau mbele isiolo. Lakini hata kama tutasema nyeri sio eneo lililotengwa, haimaanishi kuwa hakuna watu masikini sana mjini nyeri.

Kwa hivyo tusidanganywe na takwimu. Tunaambiwa kuwa Kenya ni kati ya mataifa ambapo watu wengi wana mapato wastan, lakini wengi hawawezi kununua kikombe cha chai. Hizi ni takwimu tu. Lakini hizo takwimu zapaswa kuonyesha hali halisi ya watu."

Fedha za kaunti

Haki ya kiuchumi na kijamii ni swala ambalo halijapewa uzito
​Haki ya kiuchumi na kijamii ni swala ambalo halijapewa uzitoPicha: DW/W. Mbogo

Wakazi wa maeneo yaliyokuwa yametengwa kwa muda mrefu wamelalamika jinsi fedha za kuyaimarisha maeneo hayo zinavyogawanywa wakitaka kutafsiriwa upya kwa vigezo vinavyoyatambua maeneo yaliyotengwa. Jacob Lokoi ni afisa kutoka kaunti ya Turkana na amesema:

"Tunafaa kutafsiri upya vigezo vya kuyatambua maeneo yaliyotengwa. Nakumbuka tume hii ikizuru eneo la turkana, lakini sielewi wanapotekeleza ugavi wa fedha za maeneo yaliyotengwa wanazingatia nini haswa."

Juhudi hizi zinakuja wakati viongozi nchini Kenya wakijadili marekebisho ya katiba. Seneta wa zamani Omar anahoji kwamba Wakenya na wadau wengi bado hawajaielewa na kuitekeleza ipasavyo katiba iliopo, kwa hivyo ni mapema kuanza kufikiria kuirekebisha.

 

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman