1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
BiasharaKenya

Kenya, Umoja wa Ulaya zasaini mkataba wa kibiashara

Thelma Mwadzaya19 Juni 2023

Wafanyabiashara wa Kenya wanafungua ukurasa mpya baada ya mkataba na Umoja wa Ulaya kuanza kufanya kazi. Chini ya mkataba huo, Kenya itauza bidhaa zake kwenye soko la Umoja wa Ulaya pasina vikwazo vya kodi.

https://p.dw.com/p/4SlVs
EU Kenia | William Ruto und Charles Michel
Picha: Virginia Mayo/AP Photo/picture alliance

Wakiwa kwenye ikulu ya Nairobi, Waziri wa Biashara na viwanda wa Kenya Moses Kuria, aliupongeza Umoja wa Ulaya kwa kuwa na imani na wafanyabiashara wa nchini.

Kupitia mkataba huu, bidhaa za Kenya zitapata fursa ya kuuzwa kwenye soko la Umoja wa Ulaya pasina vikwazo vya kodi na viwango. Ifahamike kuwa Kenya inauza 20% ya bidhaa zake kwenye soko la Umoja wa Ulaya na kuupa nafasi ya mshirika wake mkubwa kibiashara. Kwa upande wake, Umoja wa Ulaya utaweza kuuza kemikali na mashine kwa kufuata muongozo wa punguzo la kodi katika kipindi cha miaka 25. 

Makubaliano haya yanafikiwa wakati ambapo Umoja wa Ulaya unakabiliana na ushindani kutoka China ambayo imewekeza kwenye miradi mikubwa ya miundo mbinu barani Afrika.Mazungumzo hayo yalianza mwaka 2016 kati ya Umoja wa Ulaya na nchi 5 wanachama wa Jumuiya ya Afrika mashariki ya wakati huo ila ni Kenya pekee iliyoratibu mkataba huo.

Ulaya inawezaje kuwa mshirika wa kuaminika wa Afrika?

Hata hivyo, Umoja wa Ulaya umebainisha kuwa fursa bado ipo kwa wanachama wapya wa Jumuiya hiyo ambao ni Sudan Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kujiunga na mpango huo. Rais William Ruto na naibu wake Rigathi Gachagua walishuhudia mkataba huo ukitiwa saini kwenye ikulu ya Nairobi. Umoja wa Ulaya ni soko kubwa la bidhaa za Kenya hasa kahawa, maua, chai na mboga.

Duru zinaeleza kuwa kampuni za Umoja wa Ulaya zimewekeza zaidi ya euro bilioni 1.1 nchini Kenya katika muo go mmoja uliopita. Mkataba huu ni wa kwanza muhimu tangu 2016 kati ya Umoja wa Ulaya na taifa la Afrika. Kupitia mpango wa Global Gateway Initiative, Umoja wa Ulaya ina azma ya kuimarisha uwekezaji barani Afrika.