1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya kuwasaidia wafugaji wake kukabiliana na kiangazi

Michael Kwena 11 Oktoba 2021

Serikali ya Kenya imezindua mpango wa kununua mifugo kutoka kwa wafugaji kama njia ya kuwasaidia kukabiliana na hali ya kiangazi inayoshuhudiwa nchini humo.

https://p.dw.com/p/41WWn
Global Ideas Kenia Hirten Laikipia County
Picha: picture-alliance/Photoshot

Mwezi mmoja baada ya serikali kutangaza ukame kuwa janga la kitaifa, jamii za wafugaji kutoka majimbo kumi sasa zitashusha pumzi kufuatia hatua ya serikali kuanza kuwanunua mifugo yao wakati huu.

Waziri wa fedha na mipangilio ya serikali Ukur Yattani, amesema mpango huo utaendelea hadi pale,hali itakaporejea kuwa ya kawaida.

Waziri Yattani amesema, serikali inakusudia kuwanunua mifugo zaidi ya elfu mia moja kutoka majimbo ambayo yalitajwa kuwa katika hatari ya kuwapoteza mifugo yao kutokana na kiangazi kinachoshuhudiwa kwa sasa.

"Kwa wiki chache zijazo,serikali yetu itanunua zaidi ya ngombe elfu mia moja.Kiwanda cha nyama (KMC) kitanunua takriban ng'ombe elfu kumi na moja kutoka eneo hili,Turkana na maeneo mengine ili iwe chakula ya kuwasaidia watu na hata kuuzwa”,alisema Yattani.

Soma pia: Wakenya milioni 1.4 wakabiliwa na njaa

Ununuzi n'gombe kutoka kwa wafugaji

Uzinduzi huo uliofanyika eneo la Maikona katika eneo bunge la Horr Kaskazini, pia umebainisha kuwa, zaidi ya watu laki moja wameathirika na baa la njaa katika jimbo la Marsabit. Katibu wa kudumu katika wizara ya kilimo na idara ya mifugo Harry Kimutai, ameeleza kwamba,serikali ya kitaifa kwa ushirikiano na wadau wengine husika, iliafikia hatua hiyo ili kuwaondolea hofu jamii za wafugaji ambao wanakabiliwa na hatari ya kuwapoteza mifugo yao kutokana na kiangazi.

"Kwa mpangilio wa dharura,tuliketi kama wizara zote zinazohusika na majanga na kupitia kiwanda cha nchini nchini,serikali ikatupa milioni 450 ili tuanzishe mpango wa kununua ngombe kutoka wafuagji walioathirika”,alisema Kimutai.

Soma pia:Kenya yatenga shilingi bilioni 2 kupambana na njaa 

''Changa moto kubwa kwa sasa ni chakula''

Hali ya kiangazi imeathiri majimbo kadhaa nchini Kenya na kuhatarisha mifugo
Hali ya kiangazi imeathiri majimbo kadhaa nchini Kenya na kuhatarisha mifugoPicha: Andrew Wasike

Kwa mujibu wa kamishna wa marsabit Paul Rotich,uhaba wa mvua kwa misimu kadhaa ilizidisha hali ya sasa ya kiangazi  katika jimbo hili.

Hata hivyo,amepongeza juhudi za shirika la kukabiliana na majanga nchini NDMA kwa juhudi za zake za kuwafikia wahanga wa baa la njaa na chakula kando na fedha.

"Katika jimbo hili,jumla ya walioathirika na baa la njaa ni watu elfu mia moja na sitini.Changamoto kubwa kwa sasa ni chakula kwa binadamu,kwa mifugo na pia changamoto ya kupata maji”, alisema Rotich.

Serikali kupitia wizara ya fedha tayari imeshatoa shilingi bilioni mbili kuwasaidia wakaazi kwa kuwanunulia vyakula na maji katika maeneo yao.